24. Fadhila za kutoa


125- Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kunambia: “Toa au chinja. Usihesabu Allaah akaanza kuhesabu Anavyokupa na usizuie Allaah akaanza kuzuia kutoka kwako.”[1]

126- Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakupatapo kuombwa kitu kamwe akasema: “Hapana”.[2]

127- Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema: “Ambaye yuko na kipando cha ziada basi ampe ambaye hana kipando na ambaye yuko na chakula cha ziada ampe ambaye hana chakula.” Alifanya tukaona kuwa hakuna yeyote katika sisi ambaye yuko na haki zaidi ya kile chenye kutosheleza.”[3]

128- Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kuna mbedui alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuomba kitu ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaamrisha apewe kondoo 40.000. Mtu yule akarejea kwa watu wake na kuwaambia: “Enyi watu wangu! Ingieni katika Uislamu! Muhammad akatoa kiasi cha kwamba mtu hakhofii ufakiri tena kamwe.”[4]

129- Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Sijawahi kuona mtu baada ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ni mkarimu sana kama Mu´aawiyah.”

130- ´Urwah amesema:

“Mu´aawiyah alituma 100.000 kwa ´Aaishah. ´Aaishah hawakuwahi kusimama isipokuwa alizigawa zote. Mfanya kazi wake akaingia na kusema: “Ungeliweka dirhamu mia moja tukapata kununua nyama.” Akamwambia: “Ungenikumbusha tokea mwanzo.”

131- Mu´aawiyah alipokuwa akikutana na al-Hasan alikuwa anamwambia: “Karibu, ee mtoto wa Mtume wa Allaah” na anaamrisha apewe dirhamu 300.000. Na pindi anapokutana na Ibn-uz-Zubayr alikuwa akimwambia: “Karibu, ee binamu yake na Mtume wa Allaah” na anaamrisha apewe 100.000.

132- Hammaad bin Abiy Sulaymaan alikuwa kila siku katika Ramadhaan akifungua swawm na watu khamsini. Siku ya ´Iyd anawanunulia nguo na kila mmoja anampa 100.

133- Kuna mwanamke alikuja kwa Hassan bin Abiy Sinaan kuomba. Akamtazama na kusema: “Ee kijana! Mpe dirhamu 400.” Kukasemwa: “Ee Abu ´Abdillaah! Hivi kweli unampa dirhamu 400 mwombaji?” Akasema: “Nilivyoona alivomzuri ninachelea wanaume wengine wasije kufitinishwa naye. Ndio maana nikamtajirisha. Huenda akawepo mwanaume ambaye atapendelea kumuoa.”

134- Kuna mtu alimuomba Sa´iyd bin al-´Aasw ambapo akasema: “Ee kijana! Mpe dirhamu 500.” Mtu yule akaanza kulia. Akamuuliza: “Ni kipi kinachokuliza?” Akasema: “Ni kwa sababu ardhi huwala watu kama nyinyi.”

135- Twa´mah al-Ja´fariy amesema:

“´Imraan bin Muusa alikuwa akinitumia dinari 1000 na 2000 na akisema: “Zigawa kwa ndugu zako na usiwaambie kuwa zimetoka kwangu.”

136- Inasemekana kuwa pindi Qays bin ´Ubaadah alipopatwa na maradhi watu wachache watu ndio walimtembelea. Alipouliza sababu akaambiwa: “Wanakuonea haya kwa sababu unawadai pesa.” Akasema: “Hakuna kheri yoyote kwa pesa ambayo inanizuia mimi na ndugu zangu. Waambie kuwa madeni yote yemfutika.” Jioni kizingiti kikavunjika kwa sababu ya watu wengi waliokuja kumtembelea.

137- Bakr bin ´Abdillaah amesema:

“Ninapenda zaidi pesa ambayo inanifungamanisha na ndugu zangu. Na ninachukia zaidi pesa ambayo inaniacha nyuma.”

138- ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Muislamu bora ni yule mwenye kuunga [uhusiano], akasaidia na akanufaisha.”

139- ash-Sha´biy amesema:

“Ninampenda zaidi mtu ambaye anamuhurumia masikini, anamsaidia muhitajia, anamwangalia yatima na kumchanya msafiri kuliko mwenye kufanya ´ibaadah katika Ka´bah kwa miaka arobaini. Watu bora ni wale wenye wenye manufaa.”

[1] al-Bukhaariy (1433) na Muslim (1029).

[2] Muslim (4/1805).

[3] Muslim (12/33).

[4] Muslim (15/72)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 90-94
  • Imechapishwa: 18/03/2017