24. Da´wah ya al-Albaaniy ni kama ya wa-Saudi

Je, Da´wah ya al-Albaaniy imeenea ulimwenguni kote au ni yenye kwenda kinyume na Da´wah katika nchi hii? Bali ni yenye kuafikiana nayo. Mara nyingi anasema kuwa anaita katika Qur-aan na Sunnah kwa ufahamu wa Salaf. Vivyo hivyo ndivo wanavofanya wale wanachuoni wahakiki wa Saudi Arabia. Wanaita katika kutanguliza dalili sahihi juu ya maoni ya imamu wa madhehebu. Allaah (´Azza wa Jall) ametuamrisha kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na si mwingine yeyote. Amesema (´Azza wa ´Alaa) ikiwa ni pamoja na maneno Yake:

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” Sema: “Mtiini Allaah na Mtume, lakini mkikengeuka basi hakika Allaah hawapendi makafiri.”[1]

Kadhalika wanachuoni wahakiki wa madhehebu wanalingania na kuwa na hayo. Amepiga vita kufuata madhehebu kichwa mchunga, pasi na kujali ni madhehebu gani. Vivyo hivyo ndivo wanavofanya wanachuoni wa nchi hii. Bali maimamu wote wa madhehebu wanalingania kuchukua dalili na kutupilia mbali maoni yao yote yanayopingana na dalili. Maalik amesema:

“Hakuna yeyote mbali na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye maneno yake yanachukuliwa na kurudishwa isipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake.”[2]

ash-Shaafi´iy amesema:

“Mkisoma ndani ya kitabu changu na mkakuta kitu kinachopingana na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi fuateni Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na achaneni na maoni yangu.”[3]

Ahmad bin Hanbal amesema:

“Msinifuate kichwa mchunga. Msifuate Maalik, ash-Shaafi´iy, al-Awzaa´iy wala ath-Thawriy. Badala yake chukueni pale wanapochukua wao.”[4]

Abu Haniyfah amesema:

“Ole wako ewe Ya´quub (Abu Yuusuf)! Usiandike kila unachosikia kutoka kwangu. Mimi naweza kushika mtazamo fulani hii leo lakini nikaachana nao kesho na nikashika mtazamo fulani kesho na nikaachana nao kesho yake.”[5]

Kinachopata kufahamika ni kwamba al-Albaaniy na wanafunzi wake walichokuwa wanapinga ni ile aina fulani ya upetukaji ambapo kunatangulizwa mbele madhehebu kabla ya dalili. Mfumo huu unapigwa vita na wanachuoni wote wa Ahl-ul-Hadiyth akiwemo al-Bukhaariy na Ahmad bin Hanbal. Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mlango kuhusu mwenye kuwatii wanachuoni na viongozi katika kuharamisha aliyohalalisha au kuhalalisha aliyoharamisha Allaah amewafanya ni waungu badala ya Allaah… ´Adiy bin Haatim ameeleza kwamba alimsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisoma Aayah ifuatayo:

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ

“Wamewafanya marabi wao na watawa wao kuwa ni waungu badala ya Allaah.”[6]

Nikamwambia: “Sisi hatukuwa tukiwaabudu.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Je, hawakuwa wakiharamisha aliyoyahalalisha Allaah nanyi mkayaharamisha na wakihalalisha aliyoyaharamisha Allaah nanyi mkayahalalisha?” Nikajibu: “Ndio.” Ndipo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Huko ndio kuwaabudu.”[7]

[1] 03:31-32

[2] Ibn ´Abdil-Haadiy ameisahihisha katika ”Irshaad-us-Saalik” (1/227). Ibn ´Abdil-Barr ameipokea katika ”al-Jaami´” (2/91) na Ibn Hazm katika ”Usuul-ul-Ahkaam” (6/145) kutoka kwa al-Hakam bin ´Utaybah na Mujaahid.

[3] al-Harawiy katika  ”Dhamm-ul-Kalaam” (1/47/3), al-Khatwiyb katika ”al-Ihtijaaj bish-Shaafi´iy” (2/8), Ibn ´Asaakir (1/9/15), an-Nawawiy katika ”al-Majmuu´” (1/63), Ibn-ul-Qayyim (3/361), al-Fulaaniy, uk. 100.

[4] al-Fulaaniy (113) na Ibn-ul-Qayyim katika ”I´laam-ul-Muwaqqi´iyn” (2/302).

[5] Tazama ”al-Intiqaa’ fiy Fadhwaa-il-ith-Thalaathah al-A-immah al-Fuqahaa’”, uk. 145, ya Ibn ´Abdil-Barr.

[6] 09:31

[7] at-Tirmidhiy (3095), at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (218), al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (20137). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Ghaayat-ul-Maraam” (6).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fath ar-Rabbaaniy fiyd-Difaa´ ´an-ish-Shaykh Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy, uk. 46-49
  • Imechapishwa: 03/12/2018