1- Kujizuia kusafiri katika mwezi wa Swafar na kuacha kuanza matendo ndani yake, kama vile kuoa, jimaa na mengineyo.

2- Kuacha kusafiri pindi mwezi unapofifia na pindi mwezi unapokuwa katika alama ya nge.

3- Kuacha kusafisha nyumba wakati mtu anapokuwa katika hali ya kusafiri.

4- Mtu anaswali Rak´ah mbili wakati anapotoka kwenda katika hajj ambapo anasoma katika Rak´ah ya kwanza “al-Kaafiruun” baada ya kusoma al-Faatihah na katika Rak´ah ya pili anasoma “al-Ikhlaasw”. Anapomaliza kufanya hivo anasema:

اللهم بك انتشرت وإليك توجهت

“Ee Allaah! Hakika mimi nimetoka kwa ajili Yako na Kwako ndiko nimeelekea… “

Baada ya hapo anasoma Aayat-ul-Kursiy, Suurah al-Ikhlaasw, al-Falaq na an-Naas na nyenginezo zilizotajwa katika baadhi ya vitabu vya Fiqh.

5- Mtu kuswali Rak´ah nne.

6- Yule anayetaka kufanya hajj pindi anapotoka nyumbani kwake anasoma mwisho wa Suurah “Aal ´Imraan”, “Aayat-ul-Kursiy”, “al-Qadr” na “al-Faatihah”. Wanadai kwamba kufanya hivo kunatatua haja za duniani na Aakhirah.

7- Kumtaja Allaah na kusema “Allaahu Akbar” kwa sauti ya juu wakati mahujaji wanapoanza safari zao na pindi wanaporudi.

8- Adhaana wakati wa kuwaaga.

9- Kumfanya ngamia kutokea Misri na Syria akiwa na pazia ya Ka´bah na kusherehekea kwa kuizunguka[1].

10- Baadhi ya miji inawaaga mahujaji kwa muziki.

11- Mtu kusafiri peke yake kwa madai kwamba anaanasika kwa Allaah, kama wanavodai baadhi ya Suufiyyah.

12- Kusafiri bila ya kuchukua masurufu kwa kurekebisha madai ya kutawakali.

13- Kusafiri kwa ajili ya kutembelea makaburi ya Mitume na waja wema.

14- Mwanamume kumuoa mwanamke ambaye tayari ameshaolewa akitaka kuhiji na akawa hana Mahram. Hivyo anamuoa ili yeye ndiye awe kama Mahram wake[2].

15- Kufanya uhusiano wa kidugu baina ya mwanamke na mwanaume ambaye ni ajinabi kwake ili – kama wanavodai – awe Mahram wake. Kisha mwanaume huyo anatangamana naye mwanamke huyo kama anavyotangamana na Mahaarim zake.

16- Mwanamke kusafiri pamoja na kundi la wanawake wenzake waaminifu – kama wanavodai – pasi na kuwa na Mahram. Kwa mfano utamkuta mmoja ndiye yuko na Mahram ambapo wanadai kuwa mwanaume huyo ndiye Mahram wa wote hao.

17- Kuchukua kodi kutoka kwa mahujaji ambao wamekusudia kutekeleza faradhi ya hajj.

18- Msafiri kuswali Rak´ah mbili kila mahali anapotua. Kisha anasema:

رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلًا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ

“Ee Mola wangu! Niteremshe mteremko wenye baraka! Nawe ni Mbora wa wenye kuteremsha.”[3]

19- Msafiri kusoma Suurah “al-Ikhlaasw” mara kumi na moja kila mahali anapotua, “Aayat-ul-Kursiy” mara moja na Aayah “Hawakumuadhimisha Allaah ukweli wa kumuadhimisha![4]” mara moja.

20- Msafiri kula kitunguu saumu kila mahali atapotua.

21- Kusafiri kwenda maeneo fulani kwa ajili ya kukusudia kheri ya sehemu hiyo. Hilo halikupendekezwa na Shari´ah. Kwa mfano sehemu ambazo inasemekana kuna athari za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kama inavosemwa juu ya mwamba wa Yerusalemu, msikiti wa mguu kabla ya Dameski na makaburi ya Mitume na waja wema[5].

22- Kuzielekeza silaha wakati mtu anapofika Tabuuk.

[1] Bid´ah hii imetokomea kwa miaka mingi na himdi zote anastahiki Allaah. Hata hivyo kumekuja badala yake Bid´ah nyenginezo. Katika al-Baajuriy imekuja kwamba Ibn-ul-Qaasim amesema:

“Ni haramu kukatakata vipande ile pazia inayotambulika na pazia ya sehemu ya kusimama Ibraahiym.” (1/41)

[2] Hii na inayofuata ni miongoni mwa Bid´ah mbaya kabisa kutokana na ule udanganyifu juu ya Shari´ah na kujiweka katika kutumbukia katika madhambi mabaya.

[3] 23:29

[4] 39:66

[5] Imesihi kutoka kwa ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba aliwaona watu wakati wa hajj yake wanakimbilia sehemu fulani. Akasema: “Ni kitu gan?” Kukasemwa: “Ni msikiti ambao aliswali ndani yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).” Ndipo akasema: “Hivi ndivo walivyoangamia watu wa Kitabu pindi walipozifanya athari za Mitume wao kuwa ni masinagogi na makanisa. Yule ambaye itamtokea muda wa swalah ukamkuta huko basi na aswali. Vinginevyo asiswali.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 45-47
  • Imechapishwa: 21/07/2018