23. Wanayotakiwa kufunzwa vijana

Abu Muhammad ´Abdullaah bin Abiy Zayd al-Qayrawaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Kitu ambacho wanasihi wanaotaka ujira wanapaswa mwanzo kukitilia mkazo na kukipa kipaumbele ni kuifikisha kheri mioyoni mwa watoto wa waumini ili iweze kukita ndani yake.

MAELEZO

Wanasihi, wanafunzi na walinganizi kitu cha mwanzo wanachotakiwa kukipa kipaumbele ni kuwatilia umuhimu vijana wa waislamu, wawape maelekezo yaliyo salama na wawatenge mbali na mambo ya mpasuko na mambo ya uvyamavyama ambapo mmoja anasifiwa na mwingine anapondwa. Wanatakiwa kuwaepusha na mambo haya ambayo yamewashughulisha vijana wengi hii leo. Wanawauliza ni yepi maoni yao juu ya mtu fulani na mwanafunzi wa mtu fulani. Hii ndio shughuli yao hii leo. Hili si jambo lenye kusilihi. Waalimu wanatakiwa wawe wenye nia safi pindi wanapowafunza wanafunzi wao na wawaepushe mbali na mipasuko hii, mitihani na mambo ya kuleta tofauti. Wawaelekeze njia moja; njia ya wanachuoni na ya Salaf. Wawalee vijana kutokana na hayo. Hili ndilo la wajibu kwa mwalimu anayefunza elimu yenye manufaa. Ama yule ambaye anawafunza vijana hayo mambo mengine hakuna kingine anachofanya isipokuwa tu fitina. Anatahadharisha watu na darsa za watu na wakati huohuo anapuuza kuwafunza wanafunzi silebasi za masomo ambazo mwanafunzi mwenyewe anaweza kupambanua kati ya njia sahihi na njia isiyokuwa sahihi. Amesema:

“… wanapaswa mwanzo kukitilia mkazo na kukipa kipaumbele ni kuifikisha kheri mioyoni mwa watoto wa waumini… “

Huu ndio wajibu wa mwalimu na mlinganizi. Lengo lake anatakiwa kwanza kuifikisha kheri kwenye mioyo ya watoto wa waumini na wa waislamu. Asiwashughulishe na mambo ya tofauti ambayo yameenea hii leo kati ya vijana wa waislamu. Ni lazima kuwatilia umuhimu watoto wachanga wa waumini na kuwapa miongozo salama; kufuata Qur-aan na Sunnah kwa mfumo wa Salaf. Amesema:

“… ili iweze kukita ndani yake.”

Hili ni jambo limejaribiwa. Bado ni wenye kukumbuka yale tuliyojifunza tangu tukingali wadogo. Yale tunayoyasoma hii leo ni yenye kupotea kwa haraka. Hayashiki. Mkubwa sio kama mtoto mdogo.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 12/07/2021