23. Upindishaji wenye kusemwa vibaya

92- Inapata kubainika kuwa ni lazima kufuata njia hii yenye kusifiwa na kuacha njia nyenginezo zote. Hili linathibirisha kuwa ndio njia ya Allaah ilionyooka ambayo Yeye (Ta´ala) katuamrisha kuifuata. Nyenginezo zote ni njia za shaytwaan ambazo Allaah ametukataza kuzifuata. Baada ya hayo akayatilia mkazo hayo kwa kusema:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Kwamba hii ni njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia za vichochoro nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni kwayo mpate kumcha.”[1]

93- Endapo watasema kuwa sisi wenyewe tumepindisha maana ya Aayah na Hadiyth ikiwa ni pamoja na maneno Yake (Ta´ala):

وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ

“Naye Yu pamoja nanyi popote mlipo.”[2]

na kwamba tumefasiri kuwa ni kwa ujuzi na hivyo tumetumbukia ndani ya yaleyale kama wao,

94- tunasema kuwa sisi hatujapindisha kitu. Kufasiri matamshi haya kwa njia hiyo sio kupindisha maana. Kwa sababu kupindisha maana ni kule kulitoa tamko nje ya udhahiri wake. Maana hii ndio kinachodhihiri kutoka katika matamshi haya kwa sababu moja kwa moja ndicho kinachokuja akilini mwa mtu pindi mtu anapoisikia.

95- Udhahiri wa andiko ni kile ambacho moja kwa moja kinakuja akilini, pasi na kujali ni uhakika au majazi. Kwa ajili hiyo baadhi ya majina ya kimila, kama mfano wa (راوية) na (ظعينة), yanalenga majazi na sio uhakika. Kuyageuza kwenda katika uhakika ni kupindisha maana ambako kunahitaji dalili. Kadhalika yapo majina yenye maana ya kidini na ya uhakika wa kilugha, kama mfano wa وضوء), (طهارة), (صلاة) ,(صوم), (زكاة)) na (حج). Dhahiri ya maana ya maneno haya ni ya kidini na sio ya kilugha.

96- Yakishathibiti hayo, kitu cha kwanza ambacho mtu hufikiria pindi mtu anasema “Allaah yuko pamoja nawe”bi maana kwa kukulinda. Ndio maana Allaah akasema:

لاَ تَحْزَنْ إِنَّ اللّهَ مَعَنَا

“Usihuzunike – hakika Allaah Yu Pamoja nasi!”[3]

لَا تَخَافَا ۖ إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ

“Msikhofu, hakika Mimi niko pamoja nanyi; nasikia na naona.”[4]

Kama angekuwa anamaanisha kuwa yuko pamoja na kila mtu kwa dhati Yake, basi wasingelifanywa kuwa maalum, kwani Yeye yuko pamoja nao kila mmoja. Wala lisingempelekea Abu Bakr kuacha kuhuzunika. Kwa hivyo inapata kubainika kwamba udhahiri wa matamshi haya ni yale yaliyotajwa na kwamba sio kupindisha maana.

97- Jengine ni kwamba hata kama tutasema kuwa ni kupindisha maana, sio sisi tuliofanya hivo. Salaf, ambao imethibiti kule kupatia kwao na ikalazimika kule kuwafuata, ndio ambao wamefasiri namna hiyo. Ibn ´Abbaas, adh-Dhwahhaak, Maalik,Sufyaan na wanachuoni wengine wengi ndio waliosema kuwa Aayah inakusudia elimu Yake. Aidha imethibiti ndani ya Qur-aan, Sunnah tele na maafikiano ya Salaf kwamba Allaah (Ta´ala) yuko juu ya mbingu na juu ya ´Arshi. Aayah imetajwa kwa viashirio vinavyojulisha kuwa inalenga elimu.  Amesema (Ta´ala) mwanzoni mwake:

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ

“Je, huoni kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo mbinguni na yale yote yaliyomo ardhini?”[5]

Kisha akasema (Ta´ala) mwishoni mwake:

إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hakika Allaah juu ya kila jambo ni mjuzi.”[6]

Ameanza kwa ujuzi na akamaliza kwa ujuzi. Mtiririko wa Aayah unazungumzia kuwakhofisha juu ya elimu ya Allaah na kwamba atawafahamisha kwa yale waliyoyafanya siku ya Qiyaamah na kwamba atawalipa kwayo. Viashirio vyote hivi vinajulisha kwamba Aayah inakusudia elimu.

98- Viashirio vyote hivi, majulisho ya Hadiyth na maneno ya Salaf na maana vimeafikiana. Ni vipi basi yote hayo yatafungamanishwa na kitu kinachoenda kinyume na Qur-aan, Sunnah na maneno ya Salaf?

99- Haya ni mambo yasiyofichikana kwa yule mwenye mwenye busara – Allaah akitaka. Kama kama yalikuwa yamefichikana basi tayari nimekwishayafichua na kuyabainisha. Licha ya hivo hakuna neno endapo mtu ataacha kufasiri na kufafanua, kwa sababu hakuna ambaye amemlazimisha kuyafasiri.

[1] 06:153

[2] 57:04

[3] 09:40

[4] 20:46

[5] 58:7

[6] 58:7

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ut-Ta’wiyl, uk. 41-44
  • Imechapishwa: 11/01/2021