23. Tofauti ya Ahl-us-Sunnah na Ahl-ul-Bid´ah katika maandiko ya Sifa za Allaah

Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuzungumzwi juu ya Allaah isipokuwa kwa yale aliyojisifu Mwenyewe katika Qur-aan na yale Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyowabainishia Maswahabah zake. Hakika Yeye (Jalla Thanaa´uh) ni Mmoja:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

MAELEZO

Alipokataza majadiliano juu ya Allaah (´Azza wa Jalla) na ugomvi juu ya Majina na Sifa za Allaah, sasa anabainisha lililo la wajibu. Wajibu ni sisi kusoma Qur-aan na Sunnah na kuyapitisha kama yalivyokuja. Maana yake inachukuliwa kutoka katika lugha iliyoteremka na Qur-aan na Sunnah. Elimu maana yake kilugha inajulikana, Uso unajulikana, Jicho linajulikana, Mikono inajulikana, Kulingana na kuwa juu, yote haya yanajulikana maana yake katika lugha ya kiarabu ambayo Qur-aan imeteremshwa kwa lugha hiyo. Kuhusu Ahl-udh-Dhwalaal wanapinga na kusema kwamba hayachukuliwi kwa udhahiri wake. Wamegawanyika mafungu mawili:

La kwanza: Wamesimama na wanasema udhahiri wake sio makusudio. Wanasema kuwa hawaelewi makusudio yake. Hawa ndio Mufawwidhwah.

La pili – na hawa ndio wengi – ni Mu-awwilah. Hawa wameyafasiri kinyume na maana yake sahihi. Wao wenyewe wakapotea na wakawapoteza wengine na wakawashughulisha watu na migogoro, magomvi na majadiliano.

Lililo la wajibu ni kujisalimisha na Majina na Sifa za Allaah zilizomo ndani ya Qur-aan na Sunnah kama alivyokusudia Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kuwa Allaah Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye Mwenye kujijua na kuwajua wengine zaidi kuliko wengine. Kiumbe ambaye ni mjuzi zaidi kumjua Mola Wake ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu sisi elimu yetu ni pungufu. Sisi hatuyajui hata mengi kwa ufafanuzi yaliyomo katika nafsi zetu. Kuna mambo tusiyoyajua. Je, wewe unajua roho ni kitu gani? Unajua akili ni kitu gani? Ikiwa huyajui mambo katika kiwiliwili na nafsi yako, vipi basi utaweza kuzungumza juu ya Dhati ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ambayo hakuna mwengine anayeijua isipokuwa Yeye (Subhaanah):

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا

“Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na wala wao hawawezi kuzunguka elimu Yake.” (20:110)

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 57
  • Imechapishwa: 28/12/2017