23. Ni upi sahihi kwamba Imaam Ahmad aliswali nyuma ya Jahmiyyah?

Swali 23: Ni upi usahihi wa yale yanayonasibishwa kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) kwamba aliswali nyuma ya Jahmiyyah?

Jibu: Sijui kitu kama hicho. Imaam Ahmad alikuwa ni mmoja katika wapinzani wakubwa wa Jahmiyyah. Sijui kuwa aliswali nyuma ya Jahmiyyah[1].

Ikiwa kiongozi ana upindaji usiokuwa kufuru, ni sawa kuswali nyuma yake ni mamoja akiwa mwema au muovu. Muda  wa kuwa kiongozi hajatoka katika dini na kutumbukia ndani ya kufuru ya wazi kunaswaliwa nyuma hata kama atakuwa ni mtenda madhambi. Maswahabah waliswali nyuma ya al-Hajjaaj na viongozi wengine wenye madhambi kwa ajili tu ya kuepuka mfarakano. Hilo ni kutokamana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya kusikiliza na kutii na kutoasi[2]. Haitakiwi kuleta fitina na vurugu. Katika kufanya hivo kunaleta muungano na umoja.

[1] Mambo ni hivyo. Imethibiti kutoka kwa mwanawe ´Abdullaah ya kwamba hajuzishi kuswali nyuma ya Jahmiyyah. Amesema:

“Nilimuuliza baba yangu (Rahimahu Allaah) juu ya kuswali nyuma ya Ahl-ul-Bid´ah ambapo akajibu: “Haitakikani kuswali nyuma ya Jahmiyyah na Mu´tazilah.” (as-Sunnah (01/103))

Aliulizwa tena juu ya kuswali nyuma ya Jahmiyyah ambapo akajibu:

“Haifai kuswali nyuma yao na wala hawatakiwi kuonyeshwa heshima yoyote.” (Masaa-il-ul-Imaam Ahmad (01/63) ya Ibn Haaniy´)

Muhammad bin Yuusuf at-Twabbaa´ amesema:

“Nilimsikia mtu akimuuliza Ahmad bin Hanbal: “Ee Abu ´Abdillaah! Je, niswali nyuma ya mtu anayekunywa pombe?” Akasema: “Hapana.” Mtu yule akauliza tena:” Je, niswali nyuma ya mtu anayesema kuwa Qur-aan ni kiumbe?” Akajibu: “Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Nakukataza kuswali nyuma ya muislamu halafu waniuliza juu ya kafiri?” (ash-Shariy´ah (81) ya al-Aajurriy)

[2] Anaashiria (Hafidhwahu Allaah) Hadiyth iliyopokelewa na Muslim kupitia kwa ´Awf bin Maalik al-Ashjaa´iy kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Mwenye kutawalishiwa mtawala juu yake na akaona anamuasi Allaah, basi achukie yale anayomuasi kwayo Allaah na asiondoshe mkono wake kutoka katika utiifu.” (Muslim (1855))

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 65-66
  • Imechapishwa: 31/05/2023
  • mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy