Jina la Uislamu lilikuwa linatumika mwanzoni mwa Uislamu. Kipindi hicho kulikuwa hakutambuliki kujinasibisha katika kitu kingine mbali na Uislamu. Wakati kulipojitokeza Bid´ah, kukaenea matamanio na kila mzushi akajitenga mbali na Uislamu ndipo wema wetu waliotangulia wakalazimika kudhihirisha majina yao yaliyowekwa katika Shari´ah ambayo yanawapambanua na wapotevu wengineo. Kuanzia hapo wakaanza kujiita kwa majina yaliyopokelewa katika maandiko. Mfano wa majina hayo ni “al-Jamaa´ah” (mkusanyiko), al-Firqah an-Naajiyah” (kundi lililookoka) na at-Twaaifah al-Mansuurah” (kundi lililonusuriwa).

Vivyo hivyo wakajiita kwa yale waliyoshikamana nayo katika kutendea kazi Sunnah ambazo zimepewa mgongo na wengine. Mfano wa majina hayo ni Salaf, Ahl-ul-Hadiyth, Ahl-ul-Athar na Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

Wamejiita majina hayo kutokana na sababu nyingi. Shaykh Bakr bin ´Abdillaah Abu Zayd (Rahimahu Allaah) ametaja baadhi yake katika kitabu chake kitukufu: “Hukm-ul-Intimaa´ ilaal-Firaq wal-Ahzaab wal-Jama´aat-il-Islaamiyyah”. Miongoni mwazo:

1- Nisba hizi hazikutengana na Ummah wa Kiislamu tangu kuundwaa kwake kwa mujibu wa mfumo wa kinabii.

2- Nisba hizi zimekusanya Uislamu mzima.

3- Ni majina halisi.

4- Yamethibiti katika Sunnah Swahiyh.

5- Yako ambayo hayakutokea isipokuwa katika kuwakabili Ahl-ul-Ahwaa´ katika kurudisha Bid´ah na upotevu wao kwa ajili ya kujipambanua nao.

Utaona kuwa wakati ilipodhihiri Bid´ah basi Ah-ul-Haqq walipambanuka kwa Sunnah. Wakasema kuwa wao ni Ahl-us-Sunnah. Wakati rai iliposhika mkondo ndipo wakapambanuka kwa Hadiyth na Athar. Matokeo yake wakasema kuwa wao ni Ahl-ul-Hadiyth wal-Athar.

6- Majina haya hayawalinganii kufanya ushabiki kwa mtu mbali na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

7- Majina haya hayapelekei katika Bid´ah, maasi, kufanya ushabiki kwa mtu wala kundi fulani.

8- Kujenga kwao mapenzi na chuki, urafiki na uadui ni kutokana na Uislamu na sio kitu kingine[1].

[1] ”Hukm-ul-Intimaa´ ilaal-Firaq”, uk. 31-33

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 57-59
  • Imechapishwa: 18/08/2020