23. Mwenye busara na kujitenga kwake na watu


1- Ni wajibu kwa mwenye busara kujitenga mbali na watu na kutochanganyika nao. Lau kujitenga mbali na watu kungelikuwa hakuna sifa nyingine yenye kusifiwa isipokuwa kujiepusha na madhambi basi ingelitosha kwa mtu kutochafua usalama wake kwa kitu kinachopeleke katika mizozo.

2- ´Umar bin al-Khattwaab amesema:

“Chukueni sehemu yenu kwa kujitenga.”

3- Sufyaan bin ´Uyaynah amesema:

“Nilimuota ath-Thawriy usingizini na nikamuomba aninasihi. Akanambia: “Fanye uchache kuwatambua kwako watu. Fanye uchache kuwatambua kwako watu. Fanye uchache kuwatambua kwako watu.”

4- Ahmad bin Hanbal amesema:

“Nilimuona Ibn-us-Sammaak akimwandikia mmoja katika ndugu zake: “Lau utaweza kuhakikisha usiwe mja wa mwengine asiyekuwa isipokuwa Allaah peke yake basi ufanye hivo.”

5- Haifai kwa mwenye akili kujifanya mja wa watu mfano wake kwa kusimamia kuchunga haki zao na kuvumilia maudhi yao ikiwa ana uwezo wa kuacha kufanya hivo. Ikiwa ana uwezo wa kutochanganyika na ulimwengu basi ataweza kuutakasa moyo wake na kutouchafua muda na ´ibaadah. Wengi katika waliotangulia na waliokuja nyuma walijitenga mbali na watu kwa jumla na watu maalum.

6- Ibn-ul-Mubaarak amesema:

“al-Fudhwayl alikuja kumtembelea Daawuud Twaa-iy, lakini Daawuud akajifungua ndani. Ndipo al-Fudhwayl akakaa nje ya mlango akilia na Daawuud amekaa ndani akilia.”

7- Bakr Muhammad al-´Aabid amesema: “

“Daawuud Twaa-iy alinambia: “Ee Bakr! Jitenge mbali na watu kama jinsi unavyojitenga mbali na wanyama wakali.”

8- ´Umar bin ´Abdil-´Aziyz amesema:

“Watu waliona namna ambavyo mbwa mkubwa mweusi amelala karibu na Maalik bin Diynaar. Watu wakamwambia: “Ee Abu Yahyaa! Wewe huoni huo mbwa mkubwa alielala karibu nawe?” Akasema: “Huyu ni bora kuliko tangamano la watu wabaya.”

9- Pindi wanachuoni wakubwa kama vile Daawuud at-Twaa-iy wanapojitenga mbali na watu maalum – kama ambavyo kitendo hicho kinapelekea vilevile kujitenga na watu wa kawaida – walifanya hivo kwa ajili ya kujizoweza kusubiri juu ya upweke. Nachelea endapo mtu hatoacha kitu kilichoruhusiwa kwake basi atatumbukia katika haramu.

Kuhusiana na sababu zinazopelekea mtu kujitenga na walimwengu wote, inakuwa pale ambapo kunakuwa hakuna kheri yoyote kwao na shari ndio iliyoenea kwao. Wanazika mazuri na wanaonyesha mabaya. Mtu akiwa msomi wanasema kuwa ni mzushi. Akiwa ni mjinga wanamkejeli. Akiwa juu kuliko wao wanamuhusudu. Akiwa chini kuliko wao wanamdharau. Akizungumza wanasema kuwa anaropoka. Akinyamaza wanasema kuwa ni mpumbavu. Akihifadhi wanasema kuwa ni bakhili. Akiwa ni mtoaji wanasema kuwa ni muharibifu. Mtu mwenye kudanganyika na watu hawa mwishoni atakuja tu na atatumbukia katika ngazi zao.

10- al-Akkaaf Hafsw bin Humayd amesema:

“Nilitangamana na watu kwa miaka 50. Hakuna yeyote katika wao aliyenisitiria aibu zangu. Hakuna yeyote aliyewasiliana na mimi pindi nilipowaepuka. Sijihisi amani pindi mmoja anapoghadhibika. Kujishughulisha na watu hawa ni upumbavu mkubwa.

11- Maalik bin Anas amesema:

“Nimefikiwa na khabari ya kwamba Abu Dharr amesema: “Hapo kale watu walikuwa majani bila ya miba. Hii leo watu ni miba bila ya majani.”

12- Aliye na busara anatambua kuwa tabia za watu zinatofautiana. Kila mmoja anataka msaada na hakuna aliye tayari kujitolea. Pindi mtu anapoona kwa nduguye kitu kisichokuwa cha kawaida basi anaanza kumchukia. Mtu pindi anapochoshwa na mtu basi huanza kuona kuwa anachoshwa. Pindi mtu anapoona kuwa anachosha atamchukia. Pindi inapokuja chukia huja vilevile uadui. Ni upumbavu kwa mtu mwenye busara kujishughulisha na mtu kama huyu.

13- Mak-huul amesema:

“Ikiwa kuchanganyika na watu ni jambo zuri basi kule kuwaepuka ni salama zaidi.”

14- Maalik bin Diynaar amesema:

“Yule asiyeanasika na maneno ya Allaah na akawa anahitajia maneno ya watu ana elimu ndogo, moyo mpofu na umri uliopotea.

15- Ibraahiym al-Harbiy amesema:

“Siku moja baada ya Maghrib niliingia msikiti Mtakatifu na nikamuona al-Fudhwayl amekaa hapo. Nikamwendea na kukaa kwake. Akasema: “Ni nani?” Nikasema: “Ibraahiym.” Akasema: “Kwa nini umekuja?” Akajibu. “Nimeona uko peke yako ndio nikakujia.” Akasema: “Je, unataka kusengenya, kujipamba au kuonekana?” Akasema: “Hapana.” Akasema: “Simama utoke kwangu.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 81-85
  • Imechapishwa: 14/02/2018