23. Mke alinde heshima ya mume wake


Miongoni mwa haki za mume juu ya mke wake ni yeye kuilinda heshima yake kwa kujihifadhi yeye mwenyewe na kumhifadhia heshima yake. Kwa msemo mwingine asijiweke katika fitina. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa kuhusu wanawake bora na akajibu:

“Ni yule anayemtii mume wake pindi anapomuamrisha, anamfurahisha pindi anapomtazama na kumhifadhi juu ya nafsi yake na mali yake.”

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke yeyote atayevua nguo zake kwa mwengine asokuwa mume wake basi amevunja sitara ilioko baina yake yeye na Allaah.”[1]

Yote haya ni ili kuhifadhi heshima ya mume. Mwanamke amekatazwa hata kuvua nguo zake kwa mwengine asokuwa mume wake au mahala penye nafasi kama hiyo kama kwa mfano wote wawili kufikia na kulala sehemu fulani au wakati anapokuwa kwa familia yake akienda kwa idhini yake. La sivyo atakuwa amevunja sitara ilioko baina yake yeye na Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Usiulize juu ya watu watatu: Mtu mwenye kutengana na mkusanyiko [Jamaa´ah], kumuasi kiongozi wake na akafa hali ya kuwa ni muasi, mja mwenye kumkimbia mmliki wake na mwanamke ambaye mume wake hayupo baada ya yeye kumruzuku kwa mambo ya kidunia na halafu akavua kuonyesha mapambo yake na kuzurura mtaani wakati yeye [mume] yuko mbali.”[2]

Usiulize juu yao kwa sababu mwisho wao ni wa khatari na dhambi yao ni kubwa. Mwanamke ambaye mume wake hayuko kwa sababu anafanya kazi. Amesafiri kwenda mji mwingine ili aweze kumhudumia. Wakati yuko mbali naye anavua nguo kuonyesha mapambo na kujionyesha kwa wanaume ajinabi na kutangatanga mitaani na kumsaliti. Ni mwanamke ambaye ametumbukia katika dhambi kubwa. Kwa sababu hakuhifadhi haki ya mume wake na wala heshima yake.

Mwanamke mwema alobarikiwa anafanya kila aliwezalo ili kuhifadhi heshima ya mume wake. La sivyo anamuweka kwenye fitina ijapokuwa kwa neno moja tu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke asimguse mwanamke mwingine kwa ngozi ili amsifu kwa mume wake kana kwamba yuwamtazama.”[3]

Ikiwa haifai kwa mwanamke kumsifu mwanamke mwingine ili kuzihifadhi heshima za Waislamu na heshima ya mume wake, vipi mtu asemeje juu ya wanawake wanaowapiga picha marafiki zao wakike na kuzitundika nyumbani? Vipi mtu asemeje juu ya wanawake wanaowapiga picha wanawake wengine ili kumuonyesha mume wake?

Ikiwa ni haramu kwa mwanamke kumsifu mwanamke mwingine kwa mume wake, haina shaka yoyote ya kwamba ni haramu kwake kumuomba mume wake kwa kitu chenye kumuweka yeye au mume wake katika fitina kama mfano wa TV, mapicha, magazeti na mfano wa haya. Ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote juu ya kwamba haifai kwa mwanamke kumuomba mume wake kwa kitu kinachowaweka kwenye fitina.

[1] Abu Daawuud (4010), at-Tirmidhiy (2803), Ibn Maajah (3750) na Ahmad (6/173). Muundo ni Ibn Maajah. Nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy och Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (7/2/1296) na ”Aadaab-uz-Zafaaf”, uk. 96.

[2] Ahmad (6/96), al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad” (590), Ibn Hibbaan (10/4559) na wengine. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (542).

[3] al-Bukhaariy (5240).

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 36-38
  • Imechapishwa: 24/03/2017