23. Lililo la lazima kwa waislamu juu ya Maswahabah

Lililo la lazima kwa waislamu juu ya Maswahabah ni kuwapenda, kuwaigiliza, kuwasifia na kuwakirimu. Hayo ni kwa sababu wao ni Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao walipigana jihaad bega kwa bega pamoja naye na wakapokea elimu kutoka kwake ambapo baadaye wakawafikishia nayo Ummah (Radhiya Allaahu ´anhum). Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ

“Wale waliotangulia awali miongoni mwa Muhaajiruun na Answaar na wale waliowafuata kwa wema, Allaah ameridhika nao nao wameridhika Naye na amewaandalia mabustani yapitayo chini yake mito – ni wenye kudumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”[1]

Maneno Yake:

وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ

“… na wale waliowafuata kwa wema.”

bi maana wamewafuata, wakawaigiliza na wakapita juu ya mfumo wao kwa wema. Haiwezekani kuwafuata Maswahabah pasi na kuyajua madhehebu yao. Huku sio kuwafuata kwa wema. Wema maana yake ni kukifanya kitu vyema kabisa. Mtu hawezi kukifanya kitu vyema kabisa mpaka akitambue na kukielewa. Kwa hiyo si kila ambaye anajinasibisha kwa Maswahabah na kusema kwamba yeye yuko juu ya madhehebu ya Salaf anakuwa namna hiyo mpaka awafuate ipasavyo, jambo ambalo haliwezi kufikiwa isipokuwa mpaka mtu ajifunze. Halifikiwi kwa kule mtu kujinasibisha tu au kwa kutamani na kupenda kheri. Ni lazima kwanza ujue yale waliyokuwemo Maswahabah ujuzi mkamilifu kisha ndio uwafuate. Ama kujinasibisha pasi na kuhakikisha ni jambo halisaidii kitu. Maneno Yake:

وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ

“… na wale waliowafuata kwa wema.”

Bi maana hawakuchupa mpaka na wala hawakuzembea katika kuwafuata Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Huku ndio kuwafuata kwa wema. Kwa msemo mwingine mtu anakuwa kati ya uchupaji mpaka na uzembeaji. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

لَّقَدْ رَضِيَ اللَّـهُ عَنِ الْمُؤْمِنِينَ إِذْ يُبَايِعُونَكَ تَحْتَ الشَّجَرَةِ

“Hakika Allaah amewawia radhi waumini waliokupa kiapo cha usikivu na utiifu chini ya mti.”[2]

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّهِ وَرِضْوَانًا ۖ سِيمَاهُمْ فِي وُجُوهِهِم مِّنْ أَثَرِ السُّجُودِ ۚ ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ ۗ وَعَدَ اللَّهُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ مِنْهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

“Muhammad ni Mtume wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah. Alama zao dhahiri zi katika nyuso zao kutokana na athari za sujudu. Huu ndio wasifu wao katika Tawraat na wasifa wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake liwapendezeshe wakulima ili liwaghadhibishe makafiri. Allaah amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema katika jinsia yao maghfirah na ujira mkubwa.”[3]

Hizi ndio sifa za Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

ذَٰلِكَ مَثَلُهُمْ

“Huu ndio wasifu wao… “

Bi maana sifa zao.

فِي التَّوْرَاةِ ۚ وَمَثَلُهُمْ فِي الْإِنجِيلِ كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ

“… katika Tawraat na mfano wao katika Injiyl kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake liwapendezeshe wakulima… “[4]

Maswahabah mwanzoni ulipoanza Uislamu alikuwa mtu mmojammoja wachache. Mara ya kwanza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kujitokeza Makkah aliulizwa: “Ni nani yuko pamoja nawe juu ya dini hii?” Akajibu:

“Muungwana na mtumwa.”[5]

Muungwana alikuwa Abu Bakr. Mtumwa alikuwa Bilaal. Hali ilikuwa namna hii ulipoanza Uislamu. Hakuwa pamoja naye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa watu wachache tu. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Uislamu ulianza ni kitu kigeni na utarudi kuwa kitu kigeni kama ulivyoanza.”[6]

Uislamu ulianza katika hali hii kisha Maswahabah wakawa wengi mpaka wakafikia kiwango cha ukamilifu. Maneno Yake (Ta´ala):

كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ

“… kama mmea umetoa chipukizi lake… “

Bi maana matawi. Mbegu moja mara ya kwanza inapodhihiri inakuwa shina moja. Kisha inaota mashina zaidi na katika pande zake kunakuwa matawi mengi. Vivyo hivyo Maswahabah. Mara ya kwanza walipoanza walikuwa wachache. Kisha wakawa wengi kama mmea unavyootesha chipukizi:

كَزَرْعٍ أَخْرَجَ شَطْأَهُ فَآزَرَهُ

“… kama mmea umetoa chipukizi lake, likautia nguvu… “

Bi maana nguvu zake na likautia nguvu:

فَاسْتَغْلَظَ فَاسْتَوَىٰ عَلَىٰ سُوقِهِ

“… kisha likawa nene, kisha likasimama sawasawa juu ya shina lake… “

Likasimama juu ya mwanzi wake:

يُعْجِبُ الزُّرَّاعَ

“… liwapendezeshe wakulima… “

Kutokana na uzuri wake. Hii ndio sifa ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum).

لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ

“… liwaghadhibishe makafiri.”

Makafiri wakasirike kwa Maswahabah. Wale wanaowachukia Maswahabah ni makafiri na wanafiki. Wanachuoni wametumia dalili Aayah kwamba yule mwenye kuwachukia Maswahabah ni kafiri. Kwa sababu Allaah amesema:

لِيَغِيظَ بِهِمُ الْكُفَّارَ

“… liwaghadhibishe makafiri.”[7]

Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

لِلْفُقَرَاءِ الْمُهَاجِرِينَ الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِمْ وَأَمْوَالِهِمْ يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا وَيَنصُرُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“Wapatiwe pia mafuqara Muhaajiruun ambao wametolewa kutoka majumbani mwao na mali zao wanatafuta fadhilah na radhi kutoka kwa Allaah na wanamnusuru Allaah na Mtume Wake – hao ndio wakweli.”[8]

Amewasifia kwa sifa hizi kubwa. Kisha akasema:

أُولَـٰئِكَ هُمُ الصَّادِقُونَ

“Hao ndio wakweli.”

Kisha akasema kuhusu Answaar:

وَالَّذِينَ تَبَوَّءُوا الدَّارَ وَالْإِيمَانَ مِن قَبْلِهِمْ يُحِبُّونَ مَنْ هَاجَرَ إِلَيْهِمْ وَلَا يَجِدُونَ فِي صُدُورِهِمْ حَاجَةً مِّمَّا أُوتُوا وَيُؤْثِرُونَ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ وَلَوْ كَانَ بِهِمْ خَصَاصَةٌ ۚ وَمَن يُوقَ شُحَّ نَفْسِهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

”Na wale waliokuwa na makazi [Madiynah] na wakawa na imani kabla yao wanawapenda wale waliohajiri kwao na wala hawahisi choyo yoyote vifuani mwao kwa yale waliyopewa [Muhaajiruun] na wanawapendelea kuliko nafsi zao japokuwa wao wenyewe ni wahitaji. Na yeyote anayeepushwa na uchu wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufaulu.”[9]

Hizi ni sifa za Answaar. Aayah ya kwanza ni kuhusu Muhaajiruun na Aayah hi ni kuhusu Answaar. Halafu akasema wale waliokuja nyuma:

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ

“Na wale waliokuja baada yao… “

Aayah hii wanaingia ndani wale waliokuja baada yao mpaka siku ya Qiyaamah:

يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا

“Wanasema: “Mola wetu! Tusamehe na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa imani na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki… “

Bi maana chuki.

لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

“… kwa wale walioamini. Mola wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.”[10]

Hii ndio sifa ya Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Muhaajiruun na Answaar na wale wenye kuwafuata kwa wema mpaka siku ya Qiyaamah.

[1] 09:100

[2] 48:18

[3] 48:29

[4] 48:29

[5] Muslim (732).

[6] Muslim (145) kupitia kwa Abu Hurayrah.

[7] 48:29

[8] 59:08

[9] 59:09

[10] 59:10

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 41-44
  • Imechapishwa: 11/03/2021