23. Bid´ah za Hajj, ´Umrah na matembezi

Nimeonelea kwamba niambatanisha kwenye kitabu hiki sehemu ambapo nitaweza kutaja baadhi ya Bid´ah za hajj, matembezi ya al-Madiynah na Yerusalemu[1]. Kwa sababu watu wengi hawazijui na hivyo matokeo yake wanatumbukia ndani yake. Kwa hivyo nikapenda kuwazidishia nasaha kuzibainisha na kuwatahadharisha nazo. Kwa sababu matendo hayakubali Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) isipokuwa pale yatapokuwa ni yenye kutimiza masharti mawili:

1- Kitendo hicho kiwe kimefanywa kwa ajili ya Allaah (´Azza wa Jall) pekee.

2- Kiwe chema, hakiwezi kuwa chema isipokuwa pale kitapokuwa kimeafikiana na Sunnah na si kwenda kinyume nazo.

Ni jambo lenye kujulikana fika kwa wanachuoni wahakiki ya kwamba kila ´ibaadah yenye kudaiwa ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutuwekea nayo katika Shari´ah ya Allaah kwa maneno yake wala yeye hakujikurubisha kwayo kwa Allaah kwa matendo yake, basi ni yenye kwenda kinyume na Sunnah. Kwa kuwa kuna sampuli mbili za Sunnah:

1- Sunnah ya kimatendo (Fi´liyyah).

2- Sunnah ya kuacha (Tarkiyyah).

Zile ´ibaadah zilizoachwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi ni katika Sunnah vilevile kuziacha. Huoni kwa mfano adhaana kwa ajili ya swalah ya ´Iyd na swalah ya kumzika maiti pamoja na kuwa ni adhkari na ni kumuadhimisha Allaah (´Azza wa Jall), haisihi kwa mtu kujikurubisha kwa Allaah kwa kufanya mambo hayo. Hilo si kwa jengine isipokuwa ni kwa vile ni Sunnah kwa sababu ni mambo yaliyoachwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya yalifahamika na Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo wakatahadharisha sana kutokamana na Bid´ah matahadharisho yaliyoenea. Hudhayfah bin al-Yamaan (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kila ´ibaadah ambayo hawakuabudu kwayo Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi usiabudu kwayo.”

´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Fuata na wala usizushe. Kwani mmetoshelezwa. Lazimianeni na lile jambo la kale.”

Furaha kwa yule ambaye Allaah amemuafikisha kumtekelezea ´ibaadah kwa kumtakasia Yeye nia na kuzifuata Sunanh za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na hakuzichanganya na Bid´ah. Apate bishara njema kwa Allaah kumkubalia matendo yake na kumwingiza katika Pepo Yake – Allaah atujaalie kuwa miongoni mwa wale wanaosikia maneno na wakafuata yale yaliyo mazuri zaidi.

Tambua kuwa marejeo ya Bid´ah tulizoziashiria zinarudi katika mambo yafuatayo:

1- Hadiyth dhaifu ambazo haijuzu kuzitumia kama dalili wala kumnasibishia nazo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Sisi tunaona kuwa haifai kuzitendea kazi kutokana na yale tuliyobainisha mwanzoni mwa “Swifatu Swalaat-in-Nabiy”. Haya ndio maoni ya wanachuoni wengi. Kama mfano wa Ibn Taymiyyah na wengineo.

2- Hadiyth zilizotungwa au zisizokuwa na msingi kabisa ambazo jambo lake limefichikana kwa baadhi ya wanachuoni wa Fiqh. Matokeo yake wakajengea hukumu za dini juu yake, mambo ambayo ni miongoni mwa aina mbaya za Bid´ah na mambo yaliyozuliwa.

3- Ijtihaad na mambo ambayo baadhi ya wanachuoni wa Fiqh wameonelea kuwa ni mazuri khaswakhaswa wale wanachuoni waliokuja nyuma. Hawakuzisapoti kwa dalili za Kishari´ah. Bali wamezitaja tu kiholela na hatimaye zikachukuliwa kama Sunna yenye kufuatwa. Ni jambo lisilofichika kwa yule ambaye ana utambuzi katika dini ya kwamba jambo hilo ni katika mambo yasiyofaa kufuatwa, kwa sababu hakuna Shari´ah isipokuwa tu ile ambayo imefanywa na Allaah kuwa Shari´ah. Inatosha kwa yule ambaye mambo mbalimbali anaona na kuyafanya kuwa ni mazuri – midhali ni Mujtahid – kufaa kwake mwenyewe kuyatendea kazi yale ambayo ameonelea kuwa ni mazuri na Allaah asimuadhibu. Hata hivyo haifai kwa watu kuyafanya kuwa ni Shari´ah na Sunnah. Mtu asemeje ikiwa mambo hayo yanapingana na Sunnah yenye kutendewa kazi?

4- Desturi na mambo ya ukhurafi ambayo hayafahamishwi na Shari´ah wala akili. Mambo ni namna hii hata kama yatatendewa kazi na baadhi ya watu wajinga, wakayachukulia kuwa ni Shari´ah na yakapata watu wenye kuyasapoti ijapokuwa wakati fulani wakadai kuwa na wao ni katika wanachuoni.

Halafu inatakiwa kutambulika kuwa Bid´ah hizi hazina ukhatari wa ngazi moja. Zina daraja mbalimbali. Kuna ambazo ni kufuru na shirki ya waziwazi, kama ambavyo utajionea mwenyewe. Baadhi ya zengine ni chini ya hapo. Lakini ni wajibu kufahamu kwamba Bid´ah ndogo inayofanywa na mtu katika dini imeharamishwa baadhi ya kubainikiwa kuwa ni Bid´ah. Wako ambao wanafikiria kwamba kuna Bid´ah ambazo zimechukiwa peke yake. Si sahihi. Vipi inayumkini kuwa hivo ilihali Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kila Bid´ah ni upotevu na kila upotevu ni Motoni.”

Bi maana yule mwenye nayo.

Jambo hili limekaguliwa vilivyo na  Imaam ash-Shaatwibiy (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake kitukufu “al-I´tiswaam”. Kwa hivyo jambo la Bid´ah ni la khatari sana. Bado watu wengi ni wenye kughafilika na hilo. Hakuna wanaojua hilo isipokuwa baadhi tu ya wanachuoni. Ili uweze kutambua ukhatari wa Bid´ah utatosheka na dalili moja pale ambapo alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah ameizuia tawbah ya kila mtu wa Bid´ah mpaka pale atapoacha Bid´ah yake.”

Ameipokea at-Tawbaraaniy, adh-Dhwiyaa’ katika “al-Ahaadiyth al-Mukhtaarah” na wengineo. Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh na al-Mundhiriy ameonelea kuwa ni nzuri[2].

Nitamalizia maneno haya kwa nasaha nikiwapa wasomaji. Nasaha hii inatoka kwa Imaam mkubwa miongoni mwa wanachuoni wakubwa wa waislamu; naye si mwingine ni Shaykh Hasan bin ´Aliy al-Barbahaariy. Alikuwa ni mmoja katika watu wa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) ambaye alifariki mwaka 329. Amesema:

“Tahadhari mambo madogomadogo yaliyozuliwa, kwani hakika Bid´ah ndogondogo hupea mpaka zinakuwa kubwa. Kila Bid´ah iliyozushwa katika Ummah huu mwanzo wake ilikuwa ndogo na inafanana na haki. Hivyo akadanganyika yule aliyetumbukiaemo na matokeo yake hakuweza kutoka ndani yake. Ikapea na ikawa ni dini ambayo mtu anafuata. Natija yake mtu akaenda kinyume na Njia iliyonyooka na akatoka katika Uislamu.

Zingatia – Allaah akurehemu – kila ambaye utasikia maneno yake miongoni mwa watu wa zama zako usifanye haraka na wala usijiingize katika chochote katika hayo mpaka kwanza uulize na uchunguze: Je, Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) waliyazungumza au kuyafanya? Ukipata upokezi kutoka kwao kuhusu hayo, basi shikamana nayo. Usiyavuke na ukachagua kitu kingine ukaja kutumbukia Motoni.

Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba hautatimia Uislamu wa mja mpaka awe ni mwenye kufuata, mwenye kusadikisha na mwenye kujisalimisha. Yule mwenye kudai ya kwamba kuna jambo lolote katika Uislamu ambalo hawakututosha nalo Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), amewatuhumu uongo. Hilo litatosha kuwa ni kujitenga nao na ni kuwatukana. Ni mzushi mpotevu na mwenye kuwapoteza wengine na mwenye kuzusha katika Uislamu yasiyokuwemo.”

Allaah amrehemu Imaam Maalik pale aliposema:

“Hautofaulu mwisho wa Ummah huu isipokuwa kwa yale yaliyowafanya kwa mwanzo wao kufaulu. Yale ambayo wakati huo hayakuwa ni dini, basi leo hayawezi kuwa ni dini.”

Allaah amswalie na kumsalimu Mtume wetu aliyesema:

“Sikuacha kitu chochote kinachokukurubisheni kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni nacho. Sikuacha kitu chochote kinachokuwekeni mbali na Allaah na kukufanyeni kuukaribia Moto isipokuwa nimekukatazeni.”

[1] Tunamuomba Allaah airudishe na nchi zote za wailsamu ziwe mikononi mwa waislamu.

[2] Imetajwa katika ”Silsilah al-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (1620).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 42-45
  • Imechapishwa: 20/07/2018