23. Baadhi ya watu katika Ummah huu wataabudu masanamu


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يُؤْمِنُونَ بِالْجِبْتِ وَالطَّاغُوتِ

”Je, huzingatii wale ambao wamepewa sehemu ya Kitabu [hapo kale] wanaamini mazimwi na Twaaghuut?” (an-Nisaa´ 04:51)

2-

قُلْ هَلْ أُنَبِّئُكُم بِشَرٍّ مِّن ذَٰلِكَ مَثُوبَةً عِندَ اللَّـهِ ۚ مَن لَّعَنَهُ اللَّـهُ وَغَضِبَ عَلَيْهِ وَجَعَلَ مِنْهُمُ الْقِرَدَةَ وَالْخَنَازِيرَ وَعَبَدَ الطَّاغُوتَ

”Sema: “Je, nikujulisheni yule ambaye ni mwenye malipo mabaya zaidi kuliko haya mbele ya Allaah? Yule ambaye Allaah amemlaani na akamghadhibikia na akawafanya miongoni mwao manyani na nguruwe na wakaabudu twaaghuut.” (al-Maaidah 05:60)

3-

قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَىٰ أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا

“Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: “Bila shaka tutajenga msikiti juu yao [kama kumbukumbu]!” (al-Kahf 18:21)

 4- Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua, shibiri kwa shibiri, mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia. Wakasema: “E Mtume wa Allaah! Unamaanisha mayahudi na manaswara?” Akasema: “Kina nani wengine?”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

5- Muslim amepokea kupitia kwa at-Thawbaan (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah amenikusanyia ardhi nikaona mashariki na magharibi yake. Hakika ufalme wa Ummah wangu utafikia kiasi na vile nilivyokusanyiwa. Nimepewa hazina mbili; nyekundu na nyeupe. Mimi nimemuomba Mola wangu asiuangamize Ummah wangu kwa njaa kubwa yenye kuenea na wala asiwatumie adui akawatawalia ardhi zao isipokuwa kutokamana na wao wenyewe. Mola wangu akanambia: “Ee Muhammad! Mimi ninapotoa amri hakika hairudi wala kurejeshwa. Mimi Nimekupa wewe kwa ajili ya Ummah wako ya kwamba sintowahilikisha kwa njaa kubwa yenye kuenea na kwamba sintowatumia adui, isipokuwa kutokamana na wao wenyewe, watawalie nguvu zao wenyewe kwa wenyewe, hata kama watajikusanya watu wa pande zote za dunia wasingeliwapata, mpaka itakuwa baadhi yao wakiwaangamiza wengine na wakidhulumiana wao kwa wao.”[2]

6- al-Barqaaniy ameipokea Hadiyth hii katika “as-Swahiyh” yake na kaongezea:

“Kubwa ninalolikhofia juu ya Ummah wangu ni viongozi wenye kupoteza. Watapoanza kusimamishiana panga hazitosimamishwa mpaka siku ya Qiyaamah. Hakitosimama Qiyaamah mpaka kikundi katika Ummah wangu kiwafuate washirikina na mpaka kikundi katika Ummah wangu kiabudu masanamu. Hakika kutakuwa katika Ummah wangu waongo thelathini na kila mmoja wao atadai ya kwamba yeye ni Mtume ilihali mimi ndiye Mtume wa mwisho. Hakuna Mtume mwingine baada yangu. Hakitoacha kikundi katika Ummah wangu kuwa juu ya haki hali ya kuwa ni chenye kushinda; hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura mpaka itapofika amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”[3]

MAELEZO

Mlango unazungumzia kuhusu Hadiyth na Aayah zinazofahamisha juu ya hilo na kwamba Ummah huu haukukingwa na kutumbukia katika shirki. Kama ambavyo watu waliingia katika dini makundi kwa makundi wamekuwa pia ni wenye kutoka kwa wingi. Tayari wakati wa Abu Bakr as-Swiddiyq walikuwepo watu walioritadi kutoka katika Uislamu.

1- Allaah (Ta´ala) amesema:

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِّنَ الْكِتَابِ يُؤْمِنُونَ بِالْجِبْتِ وَالطَّاغُوتِ

”Je, huzingatii wale ambao wamepewa sehemu ya Kitabu [hapo kale] wanaamini mazimwi na Twaaghuut?”

Allaah ameeleza kwamba kuna watu katika Ahl-ul-Kitaab ambao wanaamini mazimwi, Twaaghuut na shaytwaan:

وَيَقُولُونَ لِلَّذِينَ كَفَرُواْ هَؤُلاء أَهْدَى مِنَ الَّذِينَ آمَنُواْ سَبِيلاً

“Wanasema juu ya wale ambao wamekufuru kuwa: “Hawa wameongoka zaidi katika njia kuliko wale ambao wameamini.”

Haya yalisemwa na mayahudi kama vile Ka´b bin al-Ashraf na Huyayy bin Akhtwab. Walisema kwamba Quraysh ni wenye kuongoka zaidi kuliko Muhammad na Maswahabah wake pamoja na kuwa wanatambua kuwa yuko katika haki. Walisema hivo kwa sababu ya ukaidi, hasadi, chuki na kumpinga. Wamepewa sehemu ya Kitabu lakini hata hivyo hawakuifanyia kazi. Bali wameenda kinyume nayo na wakaamini uchawi na twaaghuut na wakasema kuwa Quraysh ni wenye kuongoka njia zaidi. Ikiwa haya yaliwatokea mayahudi basi Ummah huu pia utaanguka katika hayo kutokana na Hadiyth:

“Mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua, shibiri kwa shibiri, mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia. Wakasema: “E Mtume wa Allaah! Unamaanisha mayahudi na manaswara?” Akasema: “Kina nani wengine?”

Ni dalili inayofahamisha kuwa haya ya ukafiri yatatokea katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Watapatikana wataokufuru na wenye kusema kuwa makafiri ni wenye kuongoka zaidi kuliko wafuasi wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya yametokea hapo kale na bado ni yenye kuendelea kutokea wanapatikana watu ambao wanawafadhilisha mayahudi na manaswara mbele ya Ummah huu.

2-

قُلْ هَلْ أُنَبِّئُكُم بِشَرٍّ مِّن ذَٰلِكَ مَثُوبَةً عِندَ اللَّـهِ ۚ مَن لَّعَنَهُ اللَّـهُ وَغَضِبَ عَلَيْهِ وَجَعَلَ مِنْهُمُ الْقِرَدَةَ وَالْخَنَازِيرَ وَعَبَدَ الطَّاغُوتَ

”Sema: “Je, nikujulisheni yule ambaye ni mwenye malipo mabaya zaidi kuliko haya mbele ya Allaah? Yule ambaye Allaah amemlaani na akamghadhibikia na akawafanya miongoni mwao manyani na nguruwe na wakaabudu twaaghuut.”

Ikiwa wale wa kabla yetu waliabudu waungu wa batili kama vile shaytwaan na kila chenye kuabudiwa badala ya Allaah basi kadhalika watapatikana katika Ummah huu watu watakaoabudia waungu wa batili na mizimu kutokana na Hadiyth:

“Mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua, shibiri kwa shibiri, mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia. Wakasema: “E Mtume wa Allaah! Unamaanisha mayahudi na manaswara?” Akasema: “Kina nani wengine?”

3-

قَالَ الَّذِينَ غَلَبُوا عَلَىٰ أَمْرِهِمْ لَنَتَّخِذَنَّ عَلَيْهِم مَّسْجِدًا

“Wakasema wale walioshinda katika shauri lao: “Bila shaka tutajenga msikiti juu yao [kama kumbukumbu]!”

Ikiwa katika nyumati zilizotangulia walipatikana watu waliojenga misikiti juu ya makaburi na wakaiadhimisha basi vivyo hivyo Ummah huu utakuja kufanya hivo. Haya yalitokea mwishoni mwa miaka mia moja ya mwanzo ambapo Raafidhwah wakajenga misikiti juu ya makaburi na wakaiadhimisha. Halafu kitendo chao kikaigwa na watu wanaojinasibisha na Uislamu. Hali ya waislamu ni kama ilivyotajwa katika Hadiyth:

4- Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtafuata nyayo za wale waliokuwa kabla yenu hatua kwa hatua, shibiri kwa shibiri, mpaka wakiingia shimo la mburukenge nanyi mtaingia. Wakasema: “E Mtume wa Allaah! Unamaanisha mayahudi na manaswara?” Akasema: “Kina nani wengine?”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kama jinsi wanavofanana watajifananisha makafiri kutoka katika Ummah huu  na wale makafiri waliotangulia katika kumshirikisha Allaah na kuabudu mizimu na masanamu. Kama ambavyo watu wa mwanzo waliwatukana wafuasi wa Mitume vivyo hivyo watapatikana watu katika Ummah huu kama vile Raafidhwha na Khawaarij wenye kuwatukana Maswahabah. Kila maasi na kufuru iliojitokeza kwa wale wa kale itajitokeza vilevile katika Ummah huu. Katika hayo kunaingia vilevile Hadiyth ya al-Bukhaariy kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakitosimama Qiyaamah mpaka wanawake wasongamane kulizunguka Dhul-Khilswah.”[4]

Daws ni kabila kusini mwa Ghaamid na Zahraan. Hayo yalipitika muda si mrefu sana kabla ya kutangazwa kwa nchi hii. Walikuwepo watu wanaoliabudu sanamu hili, wanalizunguka na hilo litatokea mara nyingine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakitosimama Qiyaamah mpaka wajiunge watu katika Ummah wangu na washirikina na mpaka kundi katika Ummah wangu waabudu masanamu.”[5]

 Haya pia yametokea. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hazitoenda nyusiku na michana mpaka aabudiwe al-Laat na al-´Uzzaa.”[6]

Yote haya yatatokea.

Kuna Hadiyth inayosema:

“Shaytwaan amekata tamaa ya kuabudiwa katika kisiwa cha kiarabu.”[7]

Wajinga wanatumia hoja kwa Hadiyth hii. Lakini aliyekata tamaa amekingwa na makosa? Yeye hakukingwa na makosa. Anaweza kukata tamaa juu ya kitu lakini kikatokea huko katika mustakabali. Alikata tamaa wakati alipoona dini imeshinda. Hata hivyo shirki imetokea. Kadhalika anaweza kuwa na matarajio ya kitu na kisitokee. Imesemekana vilevile kwamba amekata tamaa hali za waislamu kuwa kama zilivyokuwa hapo kabla kwa sababu kutaendelea siku zote kuwepo kundi katika Ummah huu likiwa juu ya haki. Imesemekana vilevile kwamba walengwa ni Maswahabah kutokana na upokezi “waswaliji”, bi maana Maswahabah wenye kuswali kwa sababu Allaah aliwawafikisha na akawaruzuku elimu. Maoni yote matatu ni sahihi.

5- Muslim amepokea kupitia kwa at-Thawbaan (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika Allaah amenikusanyia ardhi nikaona mashariki na magharibi yake. Hakika ufalme wa Ummah wangu utafikia kiasi na vile nilivyokusanyiwa. Nimepewa hazina mbili; nyekundu na nyeupe. Mimi nimemuomba Mola wangu asiuangamize Ummah wangu kwa njaa kubwa yenye kuenea na wala asiwatumie adui akawatawalia ardhi zao isipokuwa kutokamana na wao wenyewe. Mola wangu akanambia: “Ee Muhammad! Mimi ninapotoa amri hakika hairudi wala kurejeshwa. Mimi Nimekupa wewe kwa ajili ya Ummah wako ya kwamba sintowahilikisha kwa njaa kubwa yenye kuenea na kwamba sintowatumia adui, isipokuwa kutokamana na wao wenyewe, watawalie nguvu zao wenyewe kwa wenyewe, hata kama watajikusanya watu wa pande zote za dunia wasingeliwapata, mpaka itakuwa baadhi yao wakiwaangamiza wengine na wakidhulumiana wao kwa wao.”

Hii ni alama katika alama za utume. Ufalme wa Ummah wake ulisambaa mpaka mashariki China na mpaka magharibi kama vile Tangiee, Morocco. Lakini hata hivyo mambo hayajakuwa hivo kuhusiana na kaskazini na kusini. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nimepewa hazina mbili… “

Ni hazina ya kirumi na hazina ya kifursi. Walitawala nchi mbili kubwa; nchi ya kinaswara na nchi ya kishirikina. Haya ndio yanayotokea katika Ummah huu. Hazina zao zilitolewa katika njia ya Allaah, kama alivyokhabarisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hayo, wakati wa ukhaliyfah wa ´Umar na ´Uthmaan. Hii ni alama nyingine ya utume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi nimemuomba Mola wangu asiuangamize Ummah wangu kwa njaa kubwa yenye kuenea… “

Bi maana asiwaangamize kwa mara moja kama ilivyotokea kwa watu wa Nuuh, Swaalih na wengineo. Kwa sababu huu ndio Ummah wa mwisho. Vilevile kwa sababu ya ile kheri na baraka inayoptikana kwa Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) utabaki mpaka Qiyaamah kisimame.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… na wala asiwatumie adui akawatawalia ardhi zao isipokuwa kutokamana na wao wenyewe.”

Pindi watapoanza kutawaliana na kupigana vita wao kwa wao ndipo Allaah atawatawalishia adui wao. Haya yatatokea pindi waislamu watapofarikiana na kutofautiana. Hapo ndipo adui atatumia fursa hiyo na kuchukua yale yaliyoko mikononi mwa waislamu kwa muda mrefu.

Allaah (Ta´ala) akasema:

“Ee Muhammad! Mimi ninapotoa amri hakika hairudi wala kurejeshwa.”

Allaah anapopanga na kukadiria jambo hakuna yeyote anaweza kulizuia. Kumeshatangulia katika elimu ya Allaah ya kwamba Ummah huu kutatokea tofauti na mipasuko na kwamba du´aa yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaombea juu ya kwamba wasipigane vita na wasifarikiane baina yao haitoitikiwa. Bali amekataza du´aa hii. Kwa ajili hiyo ndio maana kumetokea mipasuko tokea wakati wa zama za kwanza na baadaye ikatokea kwa wamongoli na baadaye maadui wengine ambao walitawalia jambo la waislamu ili wasishikamane barabara na dini yao sahihi. Allaah habadilishi hali za watu mpaka wao wenyewe kwanza wazibadili hali zao. Hapa inapata kufahamika kwamba iwapo Ummah utakusanyika juu ya haki, wakanyooka kisawasawa na na wakasaidizana basi adui wao hatoweza kuwashinda. Matokeo yake Allaah ataukusanyia kheri zote. Pindi watapofarikiana na wakatofautiana basi adui wao atatumia fursa hiyo na kuwashambulia.

6- al-Barqaaniy ameipokea Hadiyth hii katika “as-Swahiyh” yake na kaongezea:

“Kubwa ninalolikhofia juu ya Ummah wangu ni viongozi wenye kupoteza. Watapoanza kusimamishiana panga hazitosimamishwa mpaka siku ya Qiyaamah. Hakitosimama Qiyaamah mpaka kikundi katika Ummah wangu kiwafuate washirikina na mpaka kikundi katika Ummah wangu kiabudu masanamu. Hakika kutakuwa katika Ummah wangu waongo thelathini na kila mmoja wao atadai ya kwamba yeye ni Mtume ilihali mimi ndiye Mtume wa mwisho. Hakuna Mtume mwingine baada yangu. Hakitoacha kikundi katika Ummah wangu kuwa juu ya haki hali ya kuwa ni chenye kushinda; hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura mpaka itapofika amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”

Hili linafidisha ukhatari wa viongozi wenye kupotosha. Nao ni wale watawala waovu. Wanafuatwa na watu wanaathirika nao na wanachukua msaada kutoka kwao katika kuyaendea mambo ya batili. Ndio maana (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alichelea juu yao. Hili linajumuisha viongozi na mahakimu wapotevu.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watapoanza kusimamishiana panga hazitosimamishwa mpaka siku ya Qiyaamah.”

Haya pia yametokea. Hii ni alama nyingine miongoni mwa alama za utume wake. Mlango wa fitina ulifunguka wakati alipouawa ´Umar. Baada ya hapo ikazidi kwa kuuawa kwa ´Uthmaan. Baada ya hapo shari ikazidi na kuzidi.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakitosimama Qiyaamah mpaka kikundi katika Ummah wangu kiwafuate washirikina na mpaka kikundi katika Ummah wangu kiabudu masanamu.”

Hii ni dalili inayothibitisha kuwa shirki itatokea katika Ummah huu, jambo ambalo limekwishatokea. Shirki imetokea katika kisiwa cha kiarabu na kwenginepo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kutakuwa katika Ummah wangu waongo thelathini na kila mmoja wao atadai ya kwamba yeye ni Mtume ilihali mimi ndiye Mtume wa mwisho.”

Hii ni alama nyingine tena ya utume. Haya pia yametokea. Mmoja wapo ni Musaylamah ambaye alidai kuwa ni Mtume na akauawa na Maswahabah. Vilevile al-Aswad al-´Ansiy mbaye naye alidai utume na akauawa wakati wa uhai wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Pia Sajaah at-Tamiymiyyah alifanya hivo lakini baadaye akatubia. Twulaykhah al-Asdiy alifanya hali kadhalika lakini baadaye akatubia. Wa mwisho wao atakuwa ad-Dajjaal ambaye kwanza atadai kuwa ni Mtume na hatimaye adai kuwa yeye ndiye Mola wa walimwengu. Hawa waliotajwa ndio wataokuwa na nguvu, mamlaka na utata. Vinginevyo wako wengi wanaodai kuwa ni Mitume. Hata hivyo baadhi yao wanasema hvio kwa sababu ya wendawazimu, upunguani na mengineyo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakitoacha kikundi katika Ummah wangu kuwa juu ya haki hali ya kuwa ni chenye kushinda; hakitodhurika na wale wenye kuwakosesha nusura mpaka itapofika amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”

Hii ni alama nyingine ya utume na ni bishara njema. Kundi hili lipo mpaka hii leo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“… mpaka itapofika amri ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).”

Bi maana mpaka pale kutapokuja upepo mzuri utaozichukua roho za waumini na mwishowe Qiyaamah kiwasimamie wale viumbe waovu kabisa. Imekuja katika baadhi ya mapokezi kwamba kikundi hicho kitakuwepo Shaam. Ikiwa mapokezi haya yamesihi basi hiyo ina maana kwamba baadhi ya nyakati na si kwamba ni daima. Lakini mapokezi yake mengi ni dhaifu. Kundi hilo halina sehemu maalum. Linaweza kuwa sehemu moja kama ambavo linaweza kuwa sehemu mbalimbali. Hakuna Hadiyth Swahiyh inayoonyesha kwamba litakuwa sehemu maalum.

[1] al-Bukhaariy (4356) na Muslim (2669).

[2] Muslim (2889).

[3] Ahmad (22448). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (1773).

[4] al-Bukhaariy (7116) na Muslim (2906).

[5] Abu Daawuud (42529, Ahmad (22448) na Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (2/289). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaami´” (1773).

[6] Muslim (2907).

[7] Muslim (2812).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 81-85
  • Imechapishwa: 12/10/2018