23. Ahl-us-Sunnah hawachukui msimamo wa kunyamaza


Lipo kundi lingine ambalo limechukua msimamo wa kutokusema kitu juu ya Qur-aan. Wanasema kwamba wanasoma Qur-aan na kunyamaza na kwamba hawasemi kuwa imeumbwa au haikuumbwa. Ndio maana wakaitwa “wasimamaji”. ´Aqiydah yao hii imezuliwa na imetokana na udhaifu na kuelewa Qur-aan na Sunnah kimakosa kuhusiana na majina na sifa za Allaah. Wameenda kinyume na Ahl-us-Sunnah. Ahl-us-Sunnah hawakusimama. Wanasema wazi kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa; imeanza Kwake na Kwake ndiko itarudi.

Kuhusiana na kutegemeza ambako ni lazima kinachotegemezwa ni namna ya dhati na sifa za Allaah. Hakuna yeyote anayejua namna ilivyo dhati na sifa Zake isipokuwa Yeye pekee. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanategemeza ujuzi wa namna ya sifa kwa Allaah. Ama kuhusu ujuzi wa maana yake wanajua, kwa sababu Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amewafunza kupitia kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameibainisha Qur-aan ikiwa ni pamoja vilevile na Aayah zinazozungumzia sifa. Hakuna yeyote katika Maswahabah ambaye alikuwa anaona kuwa haziko wazi. Hawakuwa hata wakiuliza kuzihusu kwa sababu walijua maana zake. Walikuwa ni waarabu na hivyo wanajua maana ya maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

Ahl-ul-Bid´ah pekee ndio wenye kuuliza kuhusu sifa. Kuna mtu alikuja kwa Imaam Maalik (Rahimahu Allaah) na akasema:

“Ee Abu ´Abdillaah:

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ‘Arshi.”[1]

Amelingana vipi?”

Maalik jasho zikaanza kumtoka na wasikilizaji wakasubiri wasikie nini atachosema. Kisha akasema:

“Kulingana kunajulikana. Namna haijulikani. Ni wajibu kuliamini hilo na kuuliza juu ya hilo ni Bid´ah. Nachelea wewe ni mpotevu.”

Kisha akaamrisha afukuzwe nje. Mtu huyo ameuliza namna ya kulingana, jambo ambalo ni Bid´ah. Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakuwa wakiuliza namna zilivyo sifa. Wala wale maimamu waliokuja baadaye hawakufanya hivo. Kile ambacho kilikuwa kinawatatiza walikuwa wakiuliza juu yake. Hata hivyo hawakuwa wakiuliza kuhusu mada hii kwa sababu ilikuwa wazi kabisa. Mada hii ndio elimu tukufu zaidi – ni vipi iachwe hali ya kuwa haiko wazi?

[1] 20:05

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 75-76
  • Imechapishwa: 10/10/2019