22. Tarawiyh kwa wanawake misikitini


Inafaa kwa wanawake kuhudhuria Tarawiyh msikitini kukiaminika fitina kutoka kwao na kwa sababu yao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwazuie wajakazi wa Allaah kutokamana na misikiti ya Allaah.”[1]

Isitoshe haya ndio matendo ya as-Salaf as-Swaalih (Radhiya Allaahu ´anhum). Lakini ni lazima aje hali ya kuwa ni mwenye kujisitiri, amevaa Hijaab na si mwenye kuonyesha mapambo, mwenye kujitia manukato wala si mwenye kunyanyua sauti yake wala mwenye kuonyesha mapambo. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا

“Wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika.”[2]

Kile chenye kuonekana ambacho hakuna namna ya kukificha ambacho ni ile Jilbaab, ´Abaa´ah na mfano wake. Jengine ni kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipowaamrisha wanawake kutoka kwenda kuswali siku ya ´iyd Umm ´Atwiyyah alisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Wakati mwingine mmoja wetu anakuwa hana Jilaab.” Akasema: “Amvishe dada yake katika Jilaab zake.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Sunnah kwa wanawake ni wao wajiweka nyuma ya wanaume na wajiweke mbali nao. Waanze kupanga safu kuanzia ile safu ya mwisho kwenda nyuma zaidi. Hali hiyo ni kinyume na wanaume. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Bora ya safu za wanaume ni zale za mwanzo na ovu zake ni za mwisho wake. Bora ya safu za wanawake ni zile za mwisho wake na ovu zake ni za mwanzo wake.”

Ameipokea Muslim.

Wanawake waondoke mara moja pale ambapo imamu atatoa salamu na wasichelewi isipokuwa kwa udhuru. Hilo ni kwa Hadiyth ya Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipokuwa anatoa salamu basi wanasimama wanawake pindi anapomaliza Tasliym yake na yeye anabaki mahala pake kiasi kidogo kabla hajasimama.” Akasema: “Tunaona – na Allaah ndiye mjuzi zaidi – kwamba kitendo hicho ni ili wapate kuondoka wanawake kabla hawajawawahi wanamme.”

Ameipokea al-Bukhaariy.

Ee Allaah! Tuwafikishe kwa yale uliyowafikisha watu hao na utusamehe sisi, wazazi wetu na waislamu wote kwa huruma Yako, ee Mwingi zaidi wa huruma.

Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] al-Bukhaariy na Muslim.

[2] 24:31

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 30-31
  • Imechapishwa: 16/04/2020