22. Qur-aan ni maneno ya Allaah


Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah yaliyoteremshwa na hayakuumbwa. Imetoka Kwake na itarudi Kwake. Amezungumza kwa Qur-aan kihakika. Alimzungumzia nayo Jibriyl ambapo akashuka nayo kwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haya yanathibitishwa na Qur-aan na Sunnah. Miongoni mwa dalili za Qur-aan ni pamoja na maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ

”Na ikiwa mmoja wa washirikina akikuomba umlinde, basi mlinde mpaka asikie Maneno ya Allaah.”[1]

Bi maana Qur-aan. Allaah (Ta´ala) amesema vilevile:

كِتَابٌ أَنزَلْنَاهُ إِلَيْكَ مُبَارَكٌ لِّيَدَّبَّرُوا آيَاتِهِ وَلِيَتَذَكَّرَ أُولُو الْأَلْبَابِ

“Kitabu Tumekiteremsha kwako chenye baraka ili wapate kuzingatia kwa makini Aayaat zake na ili wapate kukumbuka wenye akili.”[2]

Amesema (Ta´ala) tena:

وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ عَلَىٰ قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ

“Na hakika huu ni uteremsho wa Mola wa walimweng; ameuteremsha roho mwaminifu [na kuiingiza] kwenye moyo wako ili uwe miongoni mwa waonyaji kwa lugha ya Kiarabu ilio wazi.”[3]

Kuhusiana na dalili za Sunnah, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna awezae kunichukua kunipeleka kwa watu wake ili nifikishe maneno ya Mola Wangu? Quraysh wamenizuia kufikisha maneno ya Mola Wangu.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia al-Baraa´ bin ´Aazib:

“Unapoenda kitandani mwako sema: “Ee Allaah! Ninaisalimisha nafsi yangu Kwako. Ninauelekeza uso wangu Kwako. Ninakuachia jambo langu Wewe. Ninakutegemea Wewe kwa matarajio na khofu. Hakuna makimbilio wala uokizi isipokuwa kutoka Kwako. Ninaamini Kitabu ulichoteremsha na Mtume Wako uliyemtuma.”[5]

´Amr bin Dinaar amesema:

“Kabla ya miaka elfu sabini nimekutana na watu wakisema: “Allaah ndiye Muumbaji na vyengine vyote vimeumbwa isipokuwa Qur-aan. Qur-aan ni maneno ya Allaah na hayakuumbwa. Imetoka Kwake na itarudi Kwake.”[6]

Qur-aan imetoka Kwake ina maana ya kwamba Allaah ndiye wa kwanza kuzungumza kwayo. Hapa kuna radd kwa Jahmiyyah wanaosema kuwa Allaah aliumba maneno katika kitu kingine.

Itarudi Kwake inaweza kuwa na maana mbili:

Ya kwanza: Hakuna mwingine asiyekuwa Allaah mwenye kusifiwa kuwa amezungumza kwa Qur-aan. Yeye ndiye ambaye amezungumza kwayo na maneno ni sifa ya mzungumzaji.

Ya pili: Qur-aan itanyanyuliwa kwa Allaah (Ta´ala). Imepokelewa katika baadhi ya mapokezi ya kwamba Qur-aan itatoka kwenye misahafu na kwenye vifua na kupanda kwa Allaah. Haya yatapitika pale ambapo watu wataacha kuuitendea kazi Qur-aan kabisa kabisa. Kwa hivyo Allaah ainyanyue kutokana na kuiheshimisha – na Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] 09:06

[2] 38:29

[3] 26:192-195

[4] Abu Daawuud (4734), at-Tirmidhiy (2925), an-Nasaa’iy katika ”al-Kubraa’” (7727), Ibn Maajah (201), Ahmad (3/390) na al-Haakim (2/669) ambaye amesema kuwa ni Swahiyh. al-Haytamiy: ”Wanaume wake ni waaminifu.” (Majma´-uz-Zawaa’id (6/35))

[5] al-Bukhaariy (247) na Muslim (2710).

[6] Tazama ”as-Sunan al-Kubraa” (10/43, 205) ya al-Bayhaqiy na ”at-Tamhiyd” (24/186) ya Ibn ´Abdil-Barr.