22. Ni nani Swahabah kwa mtazamo wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah?

Mtunzi wa kitabu amesema:

“Wako kati na kati katika mlango wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… “

Maswahabah ni wingi wa Swahabah. Swahabah ni yule aliyekutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamwamini na akafa juu ya hilo. Maneno yao:

“Yule aliyekutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

anatoka ndani yake yule aliyemwamini Mtume lakini hakukutana naye. Huyu haitwi kuwa ni Swahabah. Mfano wa an-Najaashiy (Rahimahu Allaah) ambaye alimwamini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) lakini hakujaaliwa kukutana naye. Hakusemwi kuwa ni Swahabah. Wakati alipokufa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwatangazia Maswahabah zake juu ya kifo chake na akatoka nao kwenda kumswalia swalah ya ghaibu[1].

Sentesi:

“… akamwamini… “

anatoka ndani yake yule aliyekutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na asimwamini. Makafiri walikutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Walikutana naye, wakamuona na wakatangamana naye.

Sentesi:

“… akafa juu ya hilo.”

anatoka ndani yake yule aliyekutana na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), akamwamini ambapo akawa Swahabah kisha baadaye akaritadi. Katika hali hiyo unabatilika uswahabah wake na matendo yake yote kukiwemo uswahabah na mengineyo akifa juu ya kuritadi. Amesema (Ta´ala):

وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ فَأُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Atakayeritadi miongoni mwenu kutoka dini yake, akafariki hali ya kuwa ni kafiri, basi hao yameharibika matendo yao katika dunia na Aakhirah na hao ni watu wa Motoni humo ni wenye kudumu.”[2]

Lakini akitubia maoni sahihi ni kwamba Allaah anamsamehe na uswahabah wake na matendo yake yote kabla ya kuritadi yanarudi. Kwa sababu Allaah amesema:

فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ

“… akafariki hali ya kuwa ni kafiri.”

Ni dalili inayothibitisha kuwa yule mwenye kutubu na asife juu ya ukafiri matendo yake hayaharibiki. Kwa sababu Allaah ameweka sharti mbili juu ya  kuharibika kwa matendo ya mtu:

1-  Mtu aritadi.

2- Afe hali ya kuwa ni kafiri.

Huyu ndiye ambaye matendo yake yanaharibiwa katika uswahabah na mengineyo.

[1] Tazama ”Swahiyh-ul-Bukhaariy” (1245) na ”Swahiyh-ul-Muslim” (951).

[2] 02:217

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 40-41
  • Imechapishwa: 10/03/2021