22. Ni lazima yapatikane sharti hizi mbili ili ´ibaadah ikubaliwe

´Ibaadah haisihi isipokuwa kwa masharti mawili:

Ya kwanza: Kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall). Iwe imesalimika na shirki. Ikiwa iko na shirki ndani yake haikubaliwi. Amesema (Ta´ala):

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ

”Hakika umeletewa Wahy na kwa wale walio kabla yako [kwamba]: “Ukifanya shirki, bila shaka yataporomoka matendo yako.” (az-Zumar 39:65)

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangewaharibikia yale waliyokuwa wakitenda.” (al-An´aam 06:88)

Ya pili: Iwe imeafikiana na Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Isiwe ndani yake na Bid´ah na mambo mepya. Kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yule atakayefanya matendo yasiyoafikiana na amri yetu, basi itarudishwa mwenyewe.”

Bi maana kitendo hicho atarudishiwa mwenyewe.

Kwa hiyo yule mwenye kufanya kitu katika aina za ´ibaadah akamfanyia asiyekuwa Allaah anakuwa mshirikina. Hapajaliwi yule mwenye kufanyiwa. Ni mamoja ikawa ni sanamu, jiwe, mti, jini, mtu, ambaye yuhai au mfu. Mwenye kufanya kitu katika aina za ´ibaadah akamfanyia asiyekuwa Allaah anakuwa amemshirikisha Allaah (´Azza wa Jall).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 42
  • Imechapishwa: 04/07/2018