22. Mwenye busara na jinsi ya kutangamana kwake vizuri na watu

1- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

as-Salaam ni jina la Allaah na ameiweka katika ardhi. Hivyo basi ienezeni baina yenu.”

2- Ni wajibu kwa aliye na busara kueneza Salaam kwa watu wote. Mwenye kutoa Salaam  ni kama ambaye ameachia mtumwa huru. Salaam inaondosha vile vifundo vilivyofichikana na ile chuki iliyomo moyoni. Salaam inakata ususaji na inawafanya ndugu kuaminiana.

3- Mwenye kuanza kutoa Salaam anapata moja kati ya fadhila mbili; Allaah (´Azza wa Jall) anamfadhilisha juu ya yule aliyempa Salaam kwa kuwa amemkumbusha Salaam au Malaika wanamuitikia Salaam yake iwapo watu watampuuza kuiitika.

4- Zubayd al-Yaamiy amesema:

“Mkarimu zaidi katika watu ni yule mwenye kutoa kitu pasi na kutaka kulipwa kitu. Mtu anayesamehewa zaidi ni yule anayesamehe ilihali ana uwezo wa kuadhibu. Mtu bora kabisa ni yule anayemuunga yule mwenye kumkata. Bakhili kabisa katika watu ni yule mwenye kufanya ubakhili kwa Salaam.

5- Ni wajibu kwa muislamu pindi anapokutana na muislamu mwenzake amtolee Salaam akiwa ni mwenye tabasamu. Mwenye kufanya hivo yanaanguka madhambi yake kama ambavyo mtu unavyoangusha majani yake wakati wa majira ya baridi. Yule mwenye kukutana na watu akiwa na uso wenye bashasha anastahiki kurudishiwa mapenzi.

6- Tabasamu ni sifa ya wanachuoni na ya wenye hekima. Tabasamu inazima moto wa wakaidi na chuki za uchochezi. Tabasamu ni ulinzi dhidi ya wakandamizaji na inamlinda mtu kutokamana na mtu anayeharibu uhusiano kati ya watu.

7- ´Urwah amesema:

“Nimefikiwa na khabari kwamba imeandikwa katika vile vitabu vya kale: “Ee mwanangu kipenzi! Tabasamu na zungumza vizuri. Watu watakupenda zaidi kuliko kuwapa zawadi.”

 8- Haifai kwa mwenye busara ambaye ameongozwa katika wema kukutana na ambaye si mwema sawa kama yeye akiwa amekunja uso. Anatakiwa kukutana naye na uso wenye bashasha.

9- Habiyb bin Abiy Twaalib amesema:

“Katika tabia nzuri za mtu ni kuzungumza na rafiki yake hali ya kuwa ni mwenye kutabasamu.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 74-75
  • Imechapishwa: 14/02/2018