Imaam al-Barbahaariy (Rahimahu Allaah) amesema:

13- Tambua – Allaah akurehemu – ya kwamba kuchunguza kuhusu Mola ni uzushi, Bid´ah na upotevu. Hakuzungumzwi juu ya Allaah isipokuwa kwa yale aliyojisifu Mwenyewe katika Qur-aan na yale Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyowabainishia Maswahabah zake. Hakika Yeye (Jalla Thanaa´uh) ni Mmoja:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.” (42:11)

MAELEZO

Kuchunguza kuhusu Dhati ya Mola (Subhaanahu wa Ta´ala) na katika Majina na Sifa Zake ni jambo lililozushwa na wapotevu ambao hawajisalimishi juu ya maandiko na hawamchi Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Wanazungumza kuhusu Dhati ya Allaah, Majina na Sifa Zake, wanakanusha Aliyojithibitishia Allaah Mwenyewe au aliyomthibitishia Mtume Wake na wanajitolea wao wenyewe maoni na wanasema kwamba ndio sahihi. Wanazungumzia juu ya tafsiri ya maandiko kinyume na tafsiri yake sahihi au wanasema kwamba hayafahamiki na kwamba maana yake anaifahamu Allaah peke yake. Matokeo yake Maneno ya Allaah na maneno ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanakuwa kama kwamba ni ya mtu asiyefahamu kiarabu. Hapana! Hii sio haki.

Lililo la wajibu kwa wenye imani ni kuendelea na njia sahihi na njia ya wahenga wao na wawapuuze wapotevu hawa ambao wanajadili juu ya Allaah pasina hoja Aliyowaletea na wanajadili juu ya Qur-aan na Sunnah, hawana shughuli nyingine zaidi ya majadiliano. Watu hawa ni wajibu kutahadhari nao. Watu hawa sio wafuataji bali ni wazushi wanaofuata matamanio yao.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Sharh-is-Sunnah, uk. 57
  • Imechapishwa: 28/12/2017