Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msinsig wa sita:

Kurudi hoja tata ambayo ameiweka shaytwaan kwa kuacha Qur-aan na Sunnah na badala yake kufuata maoni na matamanio yenye kufarikiana na yenye kutofautiana. Nayo [maoni na matamanio yenyewe] ni kwamba Qur-aan na Sunnah hakuna mwenye kuvijua isipokuwa yule ambaye ni Mujtahid mutlaq [mwanachuoni mkubwa ambaye ana upeo wa kufanya Ijtihaad katika kila fani ya elimu]. Mujtahid ni yule mwenye kusifika na sifa kadhaa na kadhaa. Sifa ambazo huenda zisipatikane kwa ukamilifu hata kwa Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Itakapokuwa mtu hayuko hivo apuuze viwili hivyo [Qur-aan na Sunnah] kwa ulazima huo na hilo halina shaka yoyote. Na mwenye kutafuta uongofu katika hivyo [Qur-aan na Sunnah], basi ima ni zindiki au ni mwendawazimu kutokana na ugumu wa kuvifahamu. Kutakasika kutokamana na mapungufu ni kwa Allaah na himdi zote njema ni stahiki Yake. Ni mara ngapi Allaah amebainisha Kishari´ah na ki-Qadar, kimaumbile na kiamri, akijibu utata huu uliolaaniwa kwa njia mbalimbali zilizofikia kiwango cha ulazima wa ujumla:

وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Lakini watu wengi hawajui.”[1]

لَقَدْ حَقَّ الْقَوْلُ عَلَىٰ أَكْثَرِهِمْ فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ إِنَّا جَعَلْنَا فِي أَعْنَاقِهِمْ أَغْلَالًا فَهِيَ إِلَى الْأَذْقَانِ فَهُم مُّقْمَحُونَ وَجَعَلْنَا مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ سَدًّا وَمِنْ خَلْفِهِمْ سَدًّا فَأَغْشَيْنَاهُمْ فَهُمْ لَا يُبْصِرُونَ وَسَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَأَنذَرْتَهُمْ أَمْ لَمْ تُنذِرْهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ إِنَّمَا تُنذِرُ مَنِ اتَّبَعَ الذِّكْرَ وَخَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ ۖ فَبَشِّرْهُ بِمَغْفِرَةٍ وَأَجْرٍ كَرِيمٍ

“Hakika imethibiti kauli [ya adhabu] juu ya wengi wao, kwa hiyo hawaamini. Hakika Sisi tumeweka kwenye shingo zao minyororo, ikawafika videvuni [hawawezi kufanya kitu]; kwa hivyo vichwa vyao vimeinuliwa. Na tumeweka mbele yao kizuizi na nyuma yao kizuizi, hivyo tukawafunika, basi wao hawaoni. Na ni mamoja kwao, ukiwaonya au usiwaonye hawaamini. Hakika wewe unamuonya yule anayefuata ukumbusho na akamkhofu Mwingi wa rehema kwa ghaibu, basi mbashirie msamaha na ujira mtukufu.” (35:07-11)

Mwisho wake: Himdi zote ni Zake Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salaam zimwendee bwana wetu Muhammad, ahli zake na Maswahabah zake mpaka siku ya Qiyaamah.

MAELEZO

Kurudi hoja tata… – Ijtihaad katika lugha ni kutumia juhudi katika kufikia jambo gumu. Ijtihaad katika Shari´ah maana yake ni kutumia juhudi katika kufikia hukumu ya dini. Ijtihaad ina sharti ikiwa ni pamoja na:

1 – Ajue kutoka katika dalili za Shar´ah yale anayoyahitajia katika ijtihaad yake. Kama mfano wa Aayah na Hadiyth za hukumu.

2 – Ajue yale yanayohusiana na usahihi na unyonge wa Hadiyth. Kwa mfano kujua cheni ya wapokezi, wanamme wake na kadhalika.

3 – Ajue maandiko yenye kufuta, maandiko yaliyofutwa na maeneo ya maafikiano ili asije kuhukumu andiko fulani kuwa limefutwa au akaenda kinyume na maafikiano.

4 – Ajue kutoka katika dalili yale yanayoweza kuwa yanaenda kinyume na hukumu katika yale maandiko maalum, yanayofungamanisha na kadhalika ili asije kuhukumu yanayokwenda kinyume na hayo.

5 – Ajue lugha na kanuni za Fiqh yale yanayohusiana na dalili za matamko kama mfano wa maandiko yenye kuenea, maalum, yaliyoachiwa, yaliyofungamanishwa, ya jumla, yenye kubainisha na kadhalika ili aweze kuhukumu yale yanayopelekea katika dalili hizo.

6 – Awe na uwezo utakaomuwezesha kuzinyofoa hukumu kutoka katika dalili zake.

Ijtihaad imegawanyika sehemu mbalimbali na inakuwa katika mlango mmoja miongoni mwa milango ya elimu au katika moja ya masuala yake. Muhimu ni kwamba Mujtahid analazimika kutumia bidii yake katika kuitambua haki kisha baada ya hapo ahukumu kwa mujibu wa vile ilivyomdhihirikia. Akipatia, basi anapata ujira mara mbili; ujira mmoja ni kwa sababu ya ijtihaad yake na ujira mwingine ni kwa sababu ya kupatia kwake haki. Kwa sababu katika kule kupatia haki kuna kuidhihirisha na kuitendea kazi. Na akikosea basi anapata ujira mara moja na lile kosa lake linasamehewa. Amesema (Ta´ala):

“Akihukumu hakimu na akajitahidi ambapo akapatia basi anapata ujira mara mbili. Na akijitahidi na akakosea basi anapata ujira mara moja.”[2]

Itakuwa ni lazima kwake kukomeka endapo hukumu itakuwa haijamdhihirikia. Kipindi hicho itamjuzikia kufanya Taqliyq kutokana na dharurah. Amesema (Ta´ala):

فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ

“Hivyo basi waulizeni watu wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.”[3]

Shaykh-ul-Islaam bin Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Taqliyd ni sawa na kula mzoga; akiweza kunyofoa dalili kwa nafsi yake basi si halali kwake kufanya Taqliyd.”

Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika “an-Nuuniyyah”:

Elimu ni kutambua uongofu kwa dalili yake   hayo mawili ni vitu viwili haviwezi kulingana

[1] 07:187

[2] al-Bukhaariy (7352) na Muslim (1716).

[3] 16:43

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 34-36
  • Imechapishwa: 28/06/2021