22. Kaburi halijengewi simenti wala kitu kingine

Swali: Nimeona huku kwetu baadhi ya makaburi yanatengenezwa kwa simenti kwa kiasi cha urefu wa mita moja na nusu mita upana pamoja na kuandika juu yake jina la maiti, tarehe ya kufariki kwake na baadhi ya sentesi:

“Ee Allaah! Mrehemu fulani mwana wa fulani.”

Ni ipi hukumu ya mfano wa kitendo hichi[1]?

Jibu: Haijuzu kuyajengea makaburi; si kwa simenti wala kitu kingine. Aidha haijuzu kuandika juu yake. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) makatazo ya kuyajengea na kuandika juu yake. Muslim (Rahimahu Allaah) amepokea kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kulitia chokaa kaburi, kukaa juu yake na kulijengea.”[2]

Ameipokea pia at-Tirmidhiy na wengineo kwa cheni ya wapokezi Swahiyh na akazidisha:

“… na kuandika juu yake.”[3]

Isitoshe hiyo ni aina fulani ya kuchupa mpaka. Kwa hiyo ni lazima kulikemea. Uandishi pengine ukapelekea katika matokeo mabaya ambayo ni kupetuka mpaka na makatazo mengine ya ki-Shari´ah. Kinachotakiwa kufanywa ni ule mchanga kurudishwa ndani yake na linyanyuliwe takriban kiasi cha shibiri ili watu wapate kutambua kuwa ni kaburi. Hii ndio Sunnah juu ya makaburi ambayo alipita juu yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum).

Haijuzu kujenga misikiti juu yake, kuyavika mavazi wala kuweka makuba juu yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Laana ya Allaah iwe juu ya mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni sehemu ya kuswalia.”[4]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Vilevile Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Jundub bin ´Abdillaah al-Bajaliy ambaye ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) siku tano kabla hajafariki akisema:

“Hakika Allaah amenifanya kuwa kipenzi Wake wa karibu kama alivyomfanya Ibraahiym kuwa kipenzi Wake wa karibu. Na lau ningemchukua yeyote katika Ummah wangu kuwa kipenzi wangu wa karibu, basi ningelimfanya Abu Bakr kuwa kipenzi  wangu wa karibu. Tanabahini! Hakika wale waliokuwa kabla yenu walikuwa wakiyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa mahali pa kuswalia. Tanabahini! Msiyafanye makaburi kuwa mahali pa kuswalia. Hakika mimi nawakatazeni na hilo.”[5]

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Tunamwomba Allaah awawafikishe waislamu kushikamana barabara na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuthibiti juu yake na kutahadhari na yale yanayokwenda kinyume nazo. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, yukaribu.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (13/220-222).

[2] Ahmad (13736) na Muslim (970) na tamko ni lake.

[3] at-Tirmidhiy (1052), an-Nasaa´iy (2000) na Abu Daawuud (3225).

[4] Ahmad (1887), al-Bukhaariy (1390) na Muslim (529).

[5] Muslim (532).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 75-77
  • Imechapishwa: 05/05/2022