22. Dalili ya ishirini kutoka katika Sunnah kwamba Allaah yuko juu ya viumbe

20- Muhammad ametukhabarisha: Hamad ametuhadithia: Ahmad bin ´Abdillaah ametuhadithia: Sulaymaan bin Ahmad ametuhadithia: Muhammad bin Ahmad bin al-Baraa’ ametuhadithia: ´Abdul-Mun´im bin Idriys bin Sinaan ametuhadithia, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Wahb bin Munabbih, kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah na ´Abdullaah bin ´Abbaas ambao wamesema:

“´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Ukifa ni nani atakayekuosha? Utakafiniwa katika nini? Ni nani atakayekuswalia? Ni nani atakayekuingiza ndani ya kaburi?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Kuhusu kuniosha, wewe na Ibn ´Abbaas mnioshe mnimiminie maji na Jibriyl akiwa watatu wenu. Mkimaliza kuniosha basi mnikafini katika shuka tatu mpya. Jibriyl atakuja na sabuni kutoka Peponi. Mtaponiweka kwenye jeneza niwekeni msikitini na nyinyi tokeni.  Wa kwanza atakayeniswalia ni Mola wangu (´Azza wa Jall) kutoka juu ya ´Arshi Yake, kisha Jibriyl, kisha Mikaa-iyl, halafu Israafiyl, halafu Malaika, makundi kwa makundi. Baada ya hapo ingieni na mpange safu kwa safu. Asiwepo yeyote atakayenitangulia mbele yangu.” Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofariki, wakamwingiza msikitini na watu wakatoka nje. Wa kwanza kumswalia alikuwa Mola kutoka juu ya ´Arshi Yake, kisha Jibriyl, kisha Mikaa-iyl, halafu Israafiyl, halafu Malaika, makundi kwa makundi.”[1]

[1] Hilyat-ul-Awliyaa’ (4/77). adh-Dhahabiy amesema:

“Hadiyth hii imezuliwa. Naona kuwa ni katika uongo wa ´Abdul-Mun´im. Nimeipokea ili tu niweze kuharibu hali yake.” (al-´Uluww, uk. 43)

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaatu Swifat-il-´Uluww, uk. 101-102
  • Imechapishwa: 03/06/2018