21. Tofauti kati ya nguzo na jambo la wajibu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab amesema:

Ikiwa nguzo hata moja itaachwa, sawa kwa kukusudia, au kutokukusudia swalah inabatilika kwa kuiacha.

Ikiwa jambo la wajibu litaachwa kwa kukusudia, swalah yabatilika kwa kuliacha, na ikiwa litaachwa kwa kutokukusudia, itakuwa ni wajibu kuleta Sujuud-us-Sahw.

Allaah ndiye Anajua zaidi na swalah na salaam zimwendee bwana wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahaabah zake.

MAELEZO

Nguzo ikiachwa, ni mamoja ni kwa kukusudia au ni kwa kusahau, swalah inabatilika. Isipokuwa ikiwa kama ataiwahi kwa kukumbuka kwake na akarekebisha, hapo hakuna neno.

Ama mtu akiiacha nguzo kabisa na kukapita mure mrefu, anatakiwa kuirudi upya swalah yake. Lau mtu ataswali na akaacha kurukuu au kusujudu katika baadhi ya Rak´ah au akaswali pasi na kuleta Takbiyrat-ul-Ihraam anazingatiwa kuwa hakuswali. Hali kadhalika ikiwa hakukaa baina ya sajdah mbili au akafanya Sujuud moja tu ndefu au akainua kichwa chake na asiketi baina ya sajdah mbili. Ni lazima kwa mtu akae baina ya sajdah mbili. Hali kadhalika ikiwa mtu atainuka kutoka kwenye Rukuu´ na asisimame kunyooka kwa kutulizana; swalah yake si sahihi. Hali kadhalika ikiwa mtu hakusoma Tashahhud ya mwisho; swalah yake si sahihi hata kama amesahau. Vivyo hivyo ikiwa amesahau lakini kumeshapita muda mrefu.

Ambaye atasahau nguzo basi anatakiwa kuifanya na asujudu Sujuud mbili za kusahau. Kwa mfano mtu amesahau Rukuu´ katika Rak´ah ya nne na akazinduliwa; basi anatakiwa kusimama na kurukuu. Kisha akamilishe swalah yake na kusujudu Sujuud mbili za kusahau. Hali kadhalika mtu akaacha Sujuud moja wapo na akazinduliwa kabla hajasimama. Hata kama atakumbuka au atakumbushwa baada ya kusimama anatakiwa kurudi. Akikumbuka au akikumbushwa baada ya hapo, basi anatakiwa badala yake kuswali Rak´ah na asujudu Sujuud mbili za kusahau.

Kuhusu mambo ya wajibu, hakuna neno ikiwa yameachwa kwa sababu ya kusahau au kwa sababu ya ujinga. Yale yaliyosahauliwa yanatakiwa kulipizwa kwa Sujuud ya kusahau. Hivo ndivyo alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipoacha Tashahhud ya kwanza kwa sababu ya kusahau. Hali kadhalika ikiwa mtu atasahau Tasbiyh katika Rukuu´ au Sujuudu au kusema:

رَبِّ اغْفِرْ لِي

“Rabb Ighfir liy”

baina sajdah mbili au akasahau Tashahhud ya kwanza ambapo akasimama; basi anatakiwa kuleta Sujuud mbili za kusahau kabla ya kuleta Tasliym. Hili ndio la wajibu na ndio maoni yenye kuzingatiwa. Wanachuoni wengi wamesema kuwa jambo la wajibu limependekezwa tu, lakini maoni yanayosema kwamba ni wajibu ndio yenye uzito zaidi kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Swalini kama mlivyoniona nikiswali.”

Ndio maoni yaliyo na nguvu na salama zaidi.

Allaah awawafikishe wote.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mumtaaz, uk. 130
  • Imechapishwa: 15/07/2018