21. Sura ya pili: Maana ya nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake


Nguzo ya kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ina nguzo mbili. Ni pale tunaposema “Mja na Mtume Wake”. Nguzo mbili hizo zinakanusha uzembeaji na upetukaji mipaka katika haki yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ni mja na Mtume Wake. Yeye ndiye kiumbe mkamilifu zaidi juu ya sifa mbili hizi tukufu.

Mja hapa ina maana ya mmilikiwa na mtumwa. Kwa msemo mwingine ni mtu aliyeumbwa kama walivyoumbwa watu wengine na yanamfikia yale yanayowafikia. Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ

“Sema: “Hakika mimi ni mtu kama nyinyi.”[1]

Ameitekelezea (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ´ibaadah haki yake ipasavyo. Amesema (Ta´ala):

أَلَيْسَ اللَّـهُ بِكَافٍ عَبْدَهُ

”Je, kwani Allaah si Mwenye kumtosheleza mja Wake?”[2]

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي أَنزَلَ عَلَىٰ عَبْدِهِ الْكِتَابَ

“Himdi zote njema anastahiki Allaah ambaye amemteremshia mja Wake Kitabu.”[3]

سُبْحَانَ الَّذِي أَسْرَىٰ بِعَبْدِهِ لَيْلًا مِّنَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ

“Utakasifu ni wa Ambaye amemsafirisha usiku mja Wake kutoka al-Masjid al-Haraam.”[4]

Maana ya Mtume ni yule aliyetumilizwa kwa watu wote kwa ajili ya kuwalingania watu kwa Allaah hali ya kuwabashiria na kuwaonya.

Katika kumshuhudilia sifa mbili hizi ndani yake kuna kukanusha uzembeaji na upevukaji mipaka juu ya haki yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wengi miongoni mwa wale waliodai kwamba ni kaitka Ummah wake wamezembea na wamechupa mipaka katika haki yake mpaka wakamnyanyua juu zaidi ya ngazi ya utumwa kwenda katika ngazi ya kumwabudu yeye badala ya Allaah. Matokeo yake wakamtaka msaada badala ya Allaah na wakaomba kutoka kwake yale yasiyoweza yeyote isipokuwa Allaah pekee katika kutatua na kuondosha haja na majanga mbalimbali. Wengine wakakanusha ujumbe wake au wakazembea katika kumfuata na wakategemea rai na maoni mbalimbali yanayokwenda kinyume na yale aliyokuja nayo na wakapindisha maana ya khabari na hukumu zake.

[1] 18:110

[2] 39:36

[3] 18:01

[4] 17:01

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 47
  • Imechapishwa: 12/02/2020