21. Ni urahisi ulioje – tofauti kati ya Ahl-us-Sunnah na Mufawwidhwah


Lipo kundi lingine linaloitwa Mufawwidhwah (المفوضة) linalosema kwamba maana ya majina na sifa wanamtegemezea (فوضوا) Allaah na wala hawasemi kitu juu yake. Wanasoma maandiko kama yalivo na wanayaamini lakini hawathibitishi maana ya kile wanachosoma. Kwa mujibu wao wanaona kwamba Allaah pekee ndiye Mwenye kujua maana zake. Hivyo wakaitwa “Mufawwidhwah”, kwa sababu wametegemeza kitu ambacho hawakustahiki kukitegemeza. Kwani Allaah ameiteremsha Qur-aan kwa lugha ya kiarabu. Yule ambaye sio mwaramu ameamrishwa kujifunza kiarabu. Kwa sababu kiarabu ndio lugha ya Qur-aan na hivyo ameamrishwa kujifunza nayo.

Maana ya majina na sifa iko wazi kabisa. Hakuna andiko lolote linalohusu majina na sifa isipokuwa wanafunzi wanapata maana yake kama jua lilivyo wazi. Mfano wa hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

“Mwingi wa rehema amelingana juu ya ‘Arshi.”[1]

Mufawwidhwah wanasema kwamba hawazungumzii chochote juu ya maana ya Aayah hiyo. Wanachagua kuisoma pasi na kukagua maana yake.

Hata hivyo Ahl-us-Sunnah wal-Haqq wanasema Aayah maana yake ni kwamba Allaah yuko juu ya ´Arshi kihakika kwa njia inayolingana na ukubwa na utukufu Wake, pasi na kushabihisha, kufananisha, kukengeusha, kupindisha maana wala kukanusha. Ni urahisi ulioje wa kufahamu maana hii ya haki. Vivyo hivyo inahusiana na sifa zengine zote za kidhati na za kimatendo. Kwa hivyo maana iko wazi kabisa kwa kila yule mwenye kujibidisha na elimu katika Qur-aan na Sunnah kwa ufahamu wa Salaf.

[1] 20:05

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 74-75
  • Imechapishwa: 09/10/2019