Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

Inatakiwa pia kuamini kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake. Imepokelewa Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Qataadah amepokea hilo kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

al-Hakam bin Abaan amepokea hilo kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

´Aliy bin Zayd amepokea hilo kutoka kwa Yuusuf bin Mahraan, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

Tunaiamini Hadiyth hii kama ilivyo kama jinsi ilivyopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni uzushi kuzungumzia juu ya hilo. Tunaliamini kama lilivyo kama jinsi ilivyofikishwa na hatujadili na yeyote juu ya suala hili.”

MAELEZO

Zipo Hadiyth mbalimbali kuhusu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuona Mola wake hapa duniani. Miongoni mwazo ni ile iliopokelewa na Masruuq kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa). Masruuq amesema:

“Nilikuwa nimelala kwa ´Aaishah wakati aliposema: “Ee Abu ´Aaishah!  Yule mwenye kukueleza mambo matatu basi amemzulia Allaah uongo mkubwa.” Nikasema: “Yepi hayo?” Akasema: “Mwenye kusema kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemuona Mola wake basi amemzulia Allaah uongo mkubwa.” Masruuq akasema: “Nilikuwa nimekaa kwa kuegemea ambapo nikainuka na kusema: “Ee mama wa waumini! Nipe muda na usinifanyie haraka; Allaah (´Azza wa Jall) si ndiye kasema:

مَا كَذَبَ الْفُؤَادُ مَا رَأَىٰ

“Moyo haukukadhibisha yale aliyoyaona.”[1]

وَلَقَدْ رَآهُ نَزْلَةً أُخْرَىٰ

”Hakika amemuona katika uteremko mwingine?”[2]

Akasema: “Mimi ndiye wa kwanza katika Ummah huu ambaye nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na akasema: “Alikuwa Jibriyl. Sikuwahi kumuona katika umbo lake aliloumbiwa isipokuwa mara mbili hizi. Nilimuona akiteremka kutoka mbinguni. Umbo lake kubwa lilifunika yale yote yaliyoko kati ya mbingu na ardhi. Hukumskia Allaah akisema:

لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

“Macho hayamzunguki bali Yeye anayazunguka macho yote – Naye ni mpole, Mwenye khabari zote”[3]

Hukumsikia Allaah akisema:

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا فَيُوحِيَ بِإِذْنِهِ مَا يَشَاءُ ۚ إِنَّهُ عَلِيٌّ حَكِيمٌ

“Wala haikuwa kwa mtu yeyote kwamba amzungumzishe Allaah isipokuwa kwa Wahy au kutoka nyuma ya kizuizi au hutuma Mjumbe, kisha anamfunulia Wahy ayatakayo kwa idhini Yake. Hakika Yeye yuko juu kabisa,  Mwenye hekima.”[4]

Mwenye kudai kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameficha chochote katika yale Allaah aliyoteremsha juu yake, basi kwa hakika amemsemea Allaah uongo mkubwa. Kwani Allaah anasema:

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ

“Ee Mtume! Fikisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako. Na usipofanya hivo, basi utakuwa hukufikisha ujumbe Wake.”[5]

Mwenye kudai kwamba anayajua yale yatayopitika kesho basi amemsemea Allaah uongo mkubwa. Kwani Allaah anasema:

قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّـهُ ۚ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ

“Sema: Hakuna katika mbingu na ardhi yeyote ajuaye ghaibu isipokuwa Allaah na wala hawatambui lini watafufuliwa.”[6][7]

Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama amemuona Mola wake ambapo akajibu:

“Ni nuru. Ni vipi nitamuona?”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Ni nuru. Nimeiona.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Nimeona nuru.”[8]

Hadiyth hizi mbili zinatumiwa kama dalili na wale wanaosema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakumuona Mola wake usiku wa kupandishwa mbinguni.

Kuhusu yale yaliyopokelewa na at-Tirmidhiy kupitia kwa Mujaalid kutoka kwa ash-Sha´biy ambaye ameeleza:

“Ibn ´Abbaas alikutana na Ka´b ´Arafah. Akamuuliza baadhi ya maswali ambapo akapiga Takbiyr mpaka mlima ukanguruma. Ibn ´Abbaas akasema: “Sisi ni Banuu Haashim!” Ka´b akasema: “Allaah amegawanya kuonekana Kwake na maneno Yake kati ya Muhammad na Muusa. Alimzungumzisha Muusa mara mbili na Muhammad alimuona mara mbili.”[9]

hii imesimamia (Mawquuf) kwa Ibn ´Abbaas. Imekuja katika baadhi ya mapokezi kwamba amesema:

“Alimuona kwa kifua chake.”[10]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kuhusu kuonekana, imethibiti ya kwamba Ibn ´Abbaas amesema:

“Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake kwa kifua mara mbili.”

´Aaishah amepinga kuonekana. Wanachuoni wameoanisha kati ya hayo na wakasema kwamba ´Aaishah amepinga uonekanaji wa macho ilihali Ibn ´Abbaas amethibitisha uonekanaji wa kifua na hivyo hakuna mgongano wowote. Mapokezi yaliyothibiti kwa Ibn ´Abbaas ima yametajwa pasi na kufungamanishwa au kufungamanishwa kwa kifua. Mara anasema kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake. Mara husema kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola wake. Mara husema kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona. Hata hivyo haikuthibiti matamshi sahihi na ya wazi kwamba alimuona kwa macho yake.

Kadhalika Imaam Ahmad mara anataja kuonekana kwa njia isiyofungamana na mara hutaja kwa njia iliofungamana kwa moyo. Hakuna yeyote aliyesema kwamba amemsikia Imaam Ahmad akisema kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona kwa macho. Kuna baadhi ya maswahiba zake waliomsikia akisema kwa njia isiyofungamana na wanaelewa kuwa anamaanisha uonekanaji wa macho. Kadhalika wapo wengine waliomsikia Ibn ´Abbaas akizungumza kwa njia isiyofungamana na wakaelewa kuwa ni uonekanaji wa macho. Hata hivyo hakuna dalili yoyote inayoonyesha kwamba (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona kwa macho yake. Wala hilo halikuthibiti kwa yeyote katika Maswahabah. Hakuna chochote katika Sunnah kinachofahamisha juu ya hilo. Bali maandishi yaliyosihi yanakanusha hilo. Katika “as-Swahiyh” ya Muslim imekuja namna ambavyo Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) alisema:

“Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, umemuona Mola wako?” Akajibu: “Ni nuru. Ni vipi nitaiona?””[11]

Maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ni nuru. Ni vipi nitaiona?”

ni jambo linalofahamisha kuwa mbali kwa jambo hilo na kwamba nuru inayozuia kumuona. Hivyo mtu atapata kufahamu tofauti ilioko juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuona Mola wake katika safari ya usiku ya kupandishwa mbinguni.

[1] 53:11

[2] 53:13

[3] 06:103

[4] 42:51

[5] 05:67

[6] 27:65

[7] al-Bukhaariy (4855) na Muslim (177).

[8] Muslim (178).

[9] at-Tirmidhiy (3278). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (1/418).

[10] Muslim (285).

[11] Tazama ”Majmû´-ul-Fataawaa” (6/509).

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-ul-Minnah, uk. 107-110
  • Imechapishwa: 22/04/2019