21. Msingi wa sita: Mafungamano yenye nguvu na wanachuoni

6- Mafungamano ya nguvu na wanachuoni wa Sunnah

Ni jambo analolitambua kila mmoja fadhilah za wanachuoni na nafasi walionayo katika Shari´ah ya Kiislamu. Lakini baadhi ya watu wanachanganya kati ya mahimizo ya kufungamana na wanachuoni na kuwafanyia ushabiki na kuwafuata kichwa mchunga, jambo ambalo ni kosa.

Kuwa na mafungamano kwa wanachuoni ina maana ya kuchukua elimu kutoka kwao na kufaidika kutoka kwao kwa nasaha, maelekezo yao na mfano wa hayo. Inaweza vilevile kuwa na maana ya kuwaigiliza kwa wale ambao inafaa kwao kufanya hivo miongoni mwa wale watu wa kawaida na wale ambao hawana upeo wa kupambanua usawa katika mambo ya kielimu.

Jambo hili la kufungamana na wanachuoni wa Salaf tumekwishatangulia kulikariri, kuliweka wazi na kubainisha faida zake na pia kubainisha madhara yanayopelekea pindi tu wanapojiepusha nalo. Shaykh ´Abdur-Rahmaan as-Sa´diy (Rahimahu Allaah) akibainisha neema ya Allaah juu ya nchi hii:

“Allaah ameitakasa dini yenu kutokamana na Bid´ah na mambo ya shirki na amekusalimisheni na njia za shirki, njia potofu na za maangamivu na sababu alizoziwepesisha Yeye (Subhaanah) kwa njia ya kukuwekeeni kila mwanachuoni kusimama katika njia ilionyooka. Ikawa imamu wenu, ambaye ni Imaam Ahmad bin Hanbal, ndiye mwanachuoni mkubwa zaidi ambaye amenukuu Sunnah na Qur-aan. Matokeo yake kupitia yeye, marafiki zake, wafuasi zake na watu mfano wake anatambulika  Sunniy na mzushi kutoka katika mapote na makundi mengine. Mpaka Allaah akawatolea waislamu na Uislamu Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah ambaye alipambana na makafiri, wanafiki na wakanamungu wengine waliobaki. Aidha akadhihirisha na kutangaza Sunnah wazi kiasi cha kwamba wale wa mwanzo na waliokuja nyuma wakawa wanashindwa. Wanafunzi na wafuasi zake katika wanachuoni wahakiki wakaifuata njia yake. Hali iliendelea hivo mpaka akaja Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab katika nchi ya Saudi Arabia.  Akasimamia kazi hii kwa njia ya ukamilifu kabisa. Aliendelea kupambana na maadui mpaka akasimamisha Tawhiyd na Sunnah safi kati ya waja. Akaisambaratisha shirki na njia zake, Bid´ah na ufisadi. Saudi Arabia ikasalimika kutokamana na mambo hayo na badala yake ikaenea Sunnah na Tawhiyd. Kutokana na jitihadi zake zenye kushukuriwa, za wanafunzi wake na watetezi wake nchi ikasalimika na shirki. Hutopata humo kuba juu ya kaburi, kibanda chenye kutembelewa, kufanya Tawassul kwa viumbe, maulidi wala kitu kinachoabudiwa. Je, hii si ni neema ya Allaah kubwa na ihsaan Yake tukufu juu yenu kuwajaalia watukufu hawa kuwa ndio viongozi wenu ambao kupitia wao Allaah ameihifadhi dini sahihi, kuihakikisha na kuieneza mpaka nyinyi, baba zenu na watoto wenu mkakulia na huku mnakunywa kutoka katika chemchem ya Shari´ah iliosafi kabisa? Hamkuyapata haya kwa njia zenu nyinyi, kwa nguvu ya elimu na akili mlionayo. Hakika si vyenginevyo isipokuwa hayo ni fadhilah ya Allaah isiyokuwa na mwisho wala ukomo. Upande wa pili mnaona miji mbalimbali imezama ndani ya shirki, ukafiri, ukanamungu wa wazi, imejawa na Bid´ah, kujenga mabanda na makuba juu ya makaburi yanayotembelewa. Hivyo basi, mhimidini Allaah juu ya neema hizi ambazo hamuwezi kuzidhibiti wala kuzishukuru ipasavyo.”

Lau sisi tungelifungamana kikamilifu na kikosi hichi kilichobarikiwa; Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah na Imaam Ahmad (Rahimahumu Allaah), basi Allaah angetulinda kutumbukia ndani ya Bid´ah na kupinda nyuma ya mirengo batili na yenye kupotosha ambayo imejivisha vazi la Sunnah ilihali ukweli wa mambo iko mbali kabisa kutokamana na Sunnah hiyo.

Hatukuingiliwa na mapungufu haya isipokuwa pale ambapo watu waliiacha mfumo huu, wakaipiga kwenye ukuta na wakatosheka na mifumo iliotuletea watu kutoka Misri, India na kwenginepo, ambayo ni mifumo ilio mbali kabisa na mfumo wa as-Salaf as-Swaalih (Rahimahumu Allaah).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 53-55
  • Imechapishwa: 18/08/2020