21. Mke anatakiwa ayashinde mapenzi ya mume


Miongoni mwa haki za mume juu ya mke wake ayashinde mapenzi yake, amrehemu na awe ni kitulizo chake. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

“Na katika alama Zake ni kwamba Amekuumbieni kutokana na nafsi zenu [jinsi moja] wake ili mpate utulivu kwao; na Amekujaalieni baina yenu mapenzi na Rahmah. Hakika katika hayo bila shaka [kuna] alama kwa watu wanaotafakari.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanawake wenu ambao ni wanawake bora wa Peponi ni yule mwenye mahaba, mwenye rutuba na mwanamke mwenye kujirudi.”

Mwanamke alobarikiwa hujitahidi kushinda mapenzi ya mume wake kwa ulimi na maneno yake hata kama atapetuka mipaka katika hili na kudanganya kwa yale anayopenda kusikia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemruhusu mwanaume kumdanganya mke wake na mwanamke kumdanganya mume wake. Ni sawa kwa mwanamke kumdanganya mume wake na kumuonyesha mapenzi ambayo huenda hayako kabisa ndani ya moyo wake na kumfurahisha kwa yale anayopenda kusikia. Hili linaruhusiwa hata kama atadanganya.

[1] 30:21

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 34-35
  • Imechapishwa: 24/03/2017