21. Maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala)


Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wamekubaliana juu ya kwamba Allaah anazungumza na kwamba maneno Yake ni ya kihakika yanayolingana na Yeye.

Hakika (Subhaanah) anazungumza kwa herufi na sauti. Anazungumza anachotaka na wakati anapotaka. Maneno Yake ni ya sifa ya kidhati kwa njia ya kwamba daima husifika na maneno na ni sifa ya kimatendo kwa njia ya kwamba anazungumza pale anapotaka. Haya yanathibitishwa na Qur-aan na Sunnah. Allaah (Ta´ala) amesema katika Qur-aan:

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ

“Na alipokuja Muwsaa katika pahala pa miadi yetu na Mola wake Akamsemesha.”[1]

إِذْ قَالَ اللَّـهُ يَا عِيسَىٰ إِنِّي مُتَوَفِّيكَ وَرَافِعُكَ إِلَيَّ

“Aliposema Allaah: “Ee ‘Iysaa! Hakika Mimi ni Mwenye kukuchukua na Mwenye kukupandisha Kwangu.”[2]

وَنَادَيْنَاهُ مِن جَانِبِ الطُّورِ الْأَيْمَنِ وَقَرَّبْنَاهُ نَجِيًّا

”Na Tukamwita kutoka upande wa kulia wa mlima na Tukamkurubisha kuzungumza naye kwa siri.”[3]

Katika Aayah ya kwanza kuna uthibitisho kwamba maneno yanatokamana na matakwa Yake na yanatokea pale anapotaka.

Katika Aayah ya pili kuna dalili ya kwamba ni maneno ya Herufi.

Katika Aayah ya tatu kuna dalili ya kwamba ni maneno ya Sauti kwa sababu hakuwezi kupatikana wito wa kisiri pasi na sauti.

Miongoni mwa dalili za Sunnah, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Ta´ala) atamwambia: “Ee Aadaam!” Aseme: “Naitikia wito wako.” Halafu Aite kwa sauti: “Allaah anakuamrisha utoe katika dhuria yako wale watakaoenda Motoni.””[4]

Maneno Yake (Ta´ala) yana matamshi na maana. Hii ndio I´tiqaad ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya maneno ya Allaah. Maneno hayana matamshi peke yake bila ya maana na wala hayana maana peke yake bila ya matamshi. Kuhusiana na maoni ya mapote mengine, yametajwa kwa kifupi katika “Mukhtaswar-us-Swawaa´iy al-Mursalah”:

1- Karraamiyyah maoni yao ni kama ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah isipokuwa tu wao wanasema kuwa Maneno yamejitokeza baada ya kutokuwepo kwake. Wamesema hivi ili kuepuka kuthibitisha viumbe visivyokuwa na mwisho.

2- Kullaabiyyah wanaona kuwa Maneno ni maana iliyoko katika dhati Yake yaliyolazimiana naye kama mfano wa uhai na elimu. Kwa msemo mwingine ni kwamba hayatokamani na utashi Wake. Wanaonelea kuwa herufi na sauti ni hikaaya/simulizi Yake aliyoiumba ili iashirie ile maana iliyoko katika dhati Yake. Ni maana nne; maamrisho, makatazo, maelezo na utafiti.

3- Ashaa´irah wanasema kama Kullaabiyyah isipokuwa wao wanatofautiana nao katika mambo mawili:

La kwanza: Maana ya Maneno. Kullaabiyyah wanasema kuwa yana maana nne wakati Ashaa´irah wanasema kuwa yana maana moja. Kwa hivyo maelezo, utafiti, maamrisho na makatazo ni kitu kimoja na sio maneno mbali mbali. Bali yote hayo ni sifa Yake. Uhakika wa mambo ni kwamba Tawraat, Injiyl na Qur-aan vyote hivyo ni kitu kimoja. Tofauti iliopo tu ni ya ibara.

Ya pili: Kullaabiyyah wamesema kuwa herufi na sauti ni hikaaya/simulizi ya maneno ya Allaah. Ashaa´irah wamesema kuwa ni ibara ya maneno ya Allaah.

4- Saalimiyyah wanaona kuwa Maneno ni sifa iliyoko katika dhati Yake iliyolazimiana naye kama mfano wa uhai na elimu. Hivyo hayatokamani na utashi Wake. Vilevile Maneno Yake yana herufi na sauti vinavyoendana kwa wakati mmoja bila ya kitu kukitangulia kingine. Kwa mfano B S M, katika “Basmalah”, vinapitika wakati mmoja. Herufi hizi zilikuwepo daima na zitaendelea daima kuwepo.

5- Jahmiyyah na Mu´tazilah wanasema kuwa ni kiumbe na sio katika sifa za Allaah. Halafu kuna Jahmiyyah ambao wamekanusha wazi wazi Allaah kuwa na Maneno na kuna wengine ambao wameyathibtiisha lakini wakasema kuwa yameumbwa.

6- Wanafalsafa waliokuja nyuma wanaomfuata Aristo wanasema kuwa ni radoni za kiakili inayochukua nafasi katika nafsi zilizo njema na zilizo safi kutokamana na maandalizi na mapokezi yake. Maneno haya yanawajibisha taswira na mathibitisho mbali mbali kutegemea na yale maneno itakayopokea. Taswira na mathibitisho haya yanakuwa na nguvu mpaka pale yanajenga sura yenye kuangaza yanayozungumzisha kwa maneno yenye kusikika.

7- Ittihaadiyyah wanaosema kuwa kuna uwepo wa Allaah Pekee wanamaanisha kwamba maneno yote yaliyopo basi ni ya Allaah. Mmoja wao amesema:

Maneno yote yaliyopo ni Yake

Tunafanya nathati na ushairi

Maoni yote haya yanaenda kinyume na yaliyothibitishwa na Qur-aan, Sunnah na akili. Yule ambaye Allaah atamtunukia elimu na hekima ataelewa hilo.

[1] 07:143

[2] 03:55

[3] 19:52

[4] al-Bukhaariy (4741) na Muslim (222)