21. Kukaa masiku kadhaa maeneo ambapo kuko na kaburi

Swali: Katika nchi yetu kuna bwana mmoja mwema ambaye amekufa na kumejengwa kwa ajili yake maeneo juu ya kaburi lake. Kila mwaka tuko na desturi ambapo tunamwendea pamoja na watu wanamme kwa wanawake na wanabaki huko kwa muda wa siku tatu wakimsifu, wakifanya Tahliyl, Adhkaar na mengineyo katika sifa zinazotambulika. Tunataraji kutoka kwa muheshimiwa Shaykh maelekezo na miongozo.

Jibu: Kitendo hichi hakijuzu. Bali ni miongoni mwa Bid´ah zilizozuliwa na watu. Haijuzu kwa kujenga jengo juu ya kaburi lake; pasi na kujali jina litalopewa jengo hilo. Makaburi zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah zake yalikuwa wazi na hayajengewi jengo lolote. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kulijengea kaburi na kuliweka chokaa na akasema:

”Allaah awalaani mayahudi na manaswara. Wameyafanya makaburi ya Mitume wao kuwa ni mahali pa kuswalia.” [1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Jaabir al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuyatia chokaa makaburi, kukaa juu yake na kujenga juu yake.”[2]

Kujenga juu ya makaburi, kuyaweka chokaa, kuweka mapambo juu yake au pazia yote haya ni maovu na njia inayopelekea katika shirki. Haijuzu. Vivyo hivyo makuba, pazia, kujenga misikiti juu yake au taa. Hali kadhalika kuyatembelea kwa njia iliyotajwa na muulizaji; kama kukaa karibu nayo, kufanya Tahliyl, kula chakula, kuyapapasa makaburi, kuomba du´aa au kuswali karibu na kaburi yote haya ni maovu na ni Bid´ah. Hayajuzu.

Kilichowekwa katika Shari´ah ni kuyatembelea makaburi na kuwaombea du´aa kisha baada ya hapo aondoke. Ayapitie makaburi na aseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية يرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya. Allaah amrehemu aliyetangulia katika sisi na atakayekuja baadaye.”[3]

na du´aa nyenginezo mfano wake.

Haya ndio yaliyowekwa katika Shari´ah ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwafunza Maswahabah zake. Alikuwa akiwafunza pindi wanapoyatembelea makaburi waseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.”[4]

Imekuja katika Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

يرحم الله المستقدمين منا والمستأخرين

“Allaah amrehemu aliyetangulia katika sisi na atakayekuja baadaye.”

Imekuja katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas:

السلام عليكم يا أهل القبور يغفر الله لنا ولكم أنتم سلفنا ونحن بالأثر

“Amani ya Allaah iwe juu yenu enyi mliyomo ndani ya makaburi. Allaah atusamehe sisi na nyinyi. Nyinyi ni watangulizi wetu na sisi tunafuatia.”

Hiki ndio kilichowekwa katika Shari´a´h.

Ama kukaa makaburini kwa ajili ya kula, kunywa, kufanya Tahliyl, kuswali, kusoma Qur-aan yote haya ni maovu. Bali jambo la sawa ni mtu atoe salamu na aondoke zake na amwombee maiti na amtakie rehema. Ama kuyafanya ni maeneo pa kuomba du´aa, maeneo ya kusoma, maeneo ya kufanya Tahliyl au maeneo ya kula kwa muda wa siku moja au siku mbili, mambo haya hayana msingi. Isitoshe ni Bid´ah na miongoni mwa njia za shirki. Kwa hivyo ni lazima kutahadhari na kujiepusha na mambo hayo.

[1] al-Bukhaariy (436) na Muslim (529).

[2] Muslim (970).

[3] Muslim (974).

[4] Muslim (974).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 73-75
  • Imechapishwa: 05/05/2022