Allaah (Ta´ala) amesema:

فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Basi sasa waingilieni na tafuteni aliyokuandikieni Allaah. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.”[1]

Baadhi ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikosea katika hili na wakadhani kwamba inahusiana na maana yake ya kidhahiri ni kutazama tofauti kati ya uzi mweupe na uzi mweusi. Mtu alikuwa anaweza kufunga uzi mweupe kwenye mguu wake mmoja na uzi mweusi kwenye mguu wake mwingine halafu anakula na kunywa mpaka aone tofauti kati ya nyuzi hizo mbili. Kwani kipindi hicho hakukuwepo mataa. Anasitisha kula na kunywa pale anapoona tofauti kati ya nyuzi hizo mbili. ´Adiy bin Haatim (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Ee Mtume wa Allaah! Naweka nyuzi mbili chini ya mto wangu, uzi mweupe na uzi mweusi, ili niweze kubainikiwa kati ya usiku na mchana.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Basi mto wako ni mkubwa. Hilo ni giza la usiku na mwanga wa mchana.” Ina maana kwamba una mto mkubwa ikiwa kama mto wako unafunika uzi mweupe na uzi mweusi ambavyo kunakusudiwa mwanga wa alfajiri na giza la usiku. Ndipo Allaah (´Azza wa Jall) akateremsha:

حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“… mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku.”[2]

Nyongeza hii fupi:

مِنَ الْفَجْرِ

“… wa alfajiri… “

haikuteremka isipokuwa baada ya baadhi ya Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kuifahamu kimakosa Aayah. Kwa hivyo makusudio ya uzi mweupe ni mwanga wa alfajiri na uzi mweusi ni giza la usiku. Haya yakabainisha utatizi huu uliowakumba baadhi yao. Kisha Allaah (Ta´ala) akasema:

ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[3]

Hapa Allaah anabainisha mwisho wa swawm kama ambavyo mwanzoni alibainisha mwanzo wake. Lakini nini maana ya usiku? Ni sharti nyota zitokee, kama wanavyosema baadhi ya watu wa Bid´ah? Haya yanakwenda kinyume na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyomwambia swahabah wake mmoja pindi walipokuwa safarini:

“Teremka utuchanganyie.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Bado ni mchana.” Akasema: “Teremka utuchanganyie.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Bado ni mchana.” Akasema: “Teremka utuchanganyie. Pindi usiku utapofika hapa na mchana ukaenda kule basi amekwishakata swawm mfungaji.”

Bi maana hapo itakuwa inajuzu kwake kukata swawm.

[1] 02:187

[2] al-Bukhaariy (4509) na Muslim (1090).

[3] 02:187

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tafsiyr Aayaat-is-Swiyaam, uk. 37-40
  • Imechapishwa: 02/06/2017