21. Kuacha Sunnah kwa sababu imamu ni mjuzi zaidi

Hoja pekee kinzani wanayotumia ni kwamba wameiacha Sunnah kwa sababu wanamwamini imamu wa madhehebu yao na kwamba yeye ni mjuzi zaidi kuliko wao. Hili linaweza kuraddiwa kwa njia nyingi jambo ambalo litarefusha utangulizi huu. Kwa ajili hiyo mimi nitatosheka na njia moja peke yake na kusema kwamba sio imamu wa madhehebu yenu pekee ambaye ndiye mjuzi zaidi kuliko nyinyi juu ya Sunnah. Kuna mamia ya maimamu ambao ni wajuzi zaidi kuliko nyinyi juu ya Sunnah. Sunnah Swahiyh ambayo inatofautiana na madhehebu yenu ikibainika (na ikatendewa kazi na maimamu hawa), basi itakuwa ni wajibu kwenu kuitendea kazi. Hapa hoja yenu itakuwa imeanguka. Wapinzani wetu watasema kuwa nyinyi mmeifuata Sunnah hii kwa sababu mnamwamini yule imamu ambaye ameitendea kazi. Katika hali hii kumfuata ni bora kuliko kumfuata imamu anayekwenda kinyume na Sunnah. Hili ni jambo la wazi lisilofichikana kwa yeyote.

Kwa ajili hii mimi naweza kusema kwamba hakuna yeyote ambaye yuko na udhuru wa kuacha kutendea kazi kitabu hiki kilichokusanya Sunnah zilizothibiti juu ya swalah yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu ndani yake hakuna kitu ambacho wanachuoni wameafikiana juu ya kukiacha. Hakuna suala hata moja isipokuwa kuna kundi la wanachuoni wenye kuonelea hivo. Yule ambaye haonelei hivo basi ni mwenye kupewa udhuru na pia ni mwenye kupewa ujira mmoja kwa sababu ya Ijtihaad yake. Kwa sababu ima hakufikiwa na dalili kabisa au imemfikia lakini kwa njia isiyomsimamishia hoja yoyote, au kwa sababu ya udhuru wowote miongoni mwa nyudhuru zinazotambulika kwa wanachuoni. Ama yule ambaye dalili iliyothibiti itamfikia hana udhuru wowote wa kumfuata imamu wake kichwa mchunga. Bali hapa itakuwa ni wajibu kwake kufuata dalili iliyolindwa na kukosea. Hilo ndio lengo la utangulizi huu. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ۖ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ

“Enyi walioamini! Muitikieni Allaah na Mtume anapokuiteni katika yale yenye kukuhuisheni na tambueni kwamba Allaah anaingilia kati kati ya mtu na moyo wake  na kwamba Kwake mtakusanywa.”[1]

Allaah anasema haki, anaongoza katika njia iliyonyooka na Yeye pekee ndiye Mlinzi na Msaidizi bora. Ee Allaah! Msifie na umsalimu Muhammad, jamaa zake na Maswahabah zake. Himdi zote anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu.

Dameski 1381-05-20

Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy

[1] 08:24

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 64-65
  • Imechapishwa: 23/01/2019