Hukumu za nifasi ni kama hukumu za hedhi kwa haya yafuatayo:

1 – Ni haramu kumjamii mwanamke mwenye damu ya uzazi kama ilivyo haramu kumjamii mwenye hedhi na inafaa kustarehe naye mbali na kumjamii.

2 – Ni haramu kwa mwanamke mwenye damu ya uzazi kufunga, kuswali na kufanya Twawaaf kwenye Ka´bah kama ilivyo kwa mwenye hedhi.

3 – Ni haramu kwa mwanamke mwenye damu ya uzazi kugusa msahafu na kusoma Qur-aan muda wa kuwa hachelei kusahau kama ilivyo kwa mwenye hedhi.

4 – Ni wajibu kwa mwanamke mwenye damu ya uzazi kulipa swawm ya lazima kwake ambayo aliiacha kipindi cha nifasi yake kama ilivyo kwa mwenye hedhi.

5 – Ni wajibu kwa mwanamke mwenye damu ya uzazi kuoga inapoisha nifasi yake kama ilivyo wajibu kwa mwenye hedhi na dalili ya hilo ni zifuatazo:

a) Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanawake wenye damu ya uzazi walikuwa wakikaa siku arubaini.”

Ameipokea at-Tirmidhiy na wengineo.

al-Majiyd Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema katika “al-Muntaqaa’:

“Maana ya Hadiyth ni kwamba alikuwa akiamrishwa kukaa mpaka siku arubaini isije kuwa ile khabari ni uongo. Kwa sababu ada ya wanawake wa zama fulani haiwezi kukutana katika nifasi wala hedhi.”[1]

b) Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Mwanamke katika wakeze Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akikaa nifasi nyusiku arubaini ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawaamrishi kulipa swalah za kipindi cha nifasi.”

Ameipokea Abu Daawuud.

Faida:

Mwanamke mwenye damu ya uzazi ikikatika damu yake kabla ya siku arubaini ambapo akaoga, akaswali na kufunga, kisha baadaye ikamrudilia damu kabla ya siku arubaini, maoni sahihi ni kwamba inazingatiwa kuwa ni damu ya uzazi. Hivyo atakaa na zile siku alizofunga katika hali ya utwahara ni sahihi na hatozilipa tena. Tazama “Majmuu´-ul-Fataawaa”[2] ya Shaykh Muhammad bin Ibrahaiym, “al-Fataawaa”[3] ya Shaykh ´Abdul-´Aziyz bin Baaz zilizochapishwa na “Majallat-ud-Da´wah”, maelezo ya chini ya Ibn-ul-Qayyim juu ya “Sharh-uz-Zaad”[4], “ad-Dimaa’ at-Twabiy´iyyah lin-Nisaa’”[5] na “al-Fataawaa”[6] ya as-Sa´diy.

Faida nyingine:

Shaykh ´Abdur-Rahmaan as-Sa´iyd (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kutokana na yale yaliyotangulia imedhihiri kwamba damu ya uzazi sababu yake ni kuzaa na istihaadhah ni mshipa wa ugonjwa na mfano wake na kwamba damu ya hedhi ndio damu ya msingi na Allaah ndiye anajua zaidi.” Tazama kitabu “Irshaad uliyl-Baswaa-ir wal-Albaab”[7].

[1] (01/174).

[2] (02/102).

[3] (01/44).

[4] (01/405).

[5] Uk. 56055.

[6] Uk. 137.

[7] Uk. 24.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 39-41
  • Imechapishwa: 30/10/2019