21- ´Abdur-Rahmaan bin Ahmad as-Sam´aaniy ametuhadithia: Muhammad bin Ishaaq al-Qurashiy ametuhadithia: ´Uthmaan bin Sa´iyd ad-Daarimiy ametuhadithia: ´Abdullaah bin Swaalih ametuhadithia: Yahyaa bin Ayyuub amenihadithia, kutoka kwa Ibn Jariyr, kutoka kwa ´Atwaa´ bin Abiy Rabaah, kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Aadam (´alayhis-Salaam) alikuwa akisabihi na akiswali kama wanavyosabihi na wanavyoswali Malaika pindi alipoteremka katika ardhi, kwa sababu ya urefu wake na ukaribu wake na mbingu. Lakini Allaah akaweka mkono Wake juu yake akapungua dhiraa 70.”[1]

[1] ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy amesema:

”Sikujaaliwa kupata wasifu wa mwalimu wa mwandishi – ´Abdur-Rahmaan as-Sam´aaniy – wala wasifu wa mwalimu wa mwalimu wake. Tamko la Hadiyth ni geni. Katika mlolongo wa wapokezi kuna wapokezi ambao wanatambulika kukosea sana. Hadiyth sio Swahiyh, imeshabihiana sana na yenye kuzuliwa. Kuna dalili za kutosheleza katika Qur-aan na Sunnah Swahiyh zinazothibitisha sifa hii kwa njia inayolingana na utukufu na ukamilifu Wake. Katika Aayah za Qur-aan ni pamoja na maneno Yake (Ta´ala):

وَقَالَتِ الْيَهُودُ يَدُ اللَّـهِ مَغْلُولَةٌ ۚ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا بِمَا قَالُوا ۘ بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ

”Mayahudi wakasema: “Mkono wa Allaah umefumbwa.” Mikono yao ndio iliyofumbwa na wamelaaniwa kwa yale waliyoyasema. Bali mikono Yake imekunjuliwa hutoa atakavyo.” (05:64)

Abuu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuwa Aadam alimwambia Muusa (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam):

”Wewe ndiye Muusa. Allaah amekuteua kwa maneno Yake na akakuandikia kwa mkono Wake.” (al-Bukhaariy (6614) na Muslim (2652)) (al-Arba´uun fiy Dalaa-il-it-Tawhiyd, uk. 68-69)

  • Mhusika: Imaam Abu Ismaa´iyl ´Abdullaah bin Muhammad al-Answaariy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Arba´uun fiy Dalaa-il-it-Tawhiyd, uk. 50
  • Imechapishwa: 26/01/2017