21. Dalili juu ya kwamba inajuzu kwa mwanamke kuonesha uso

Nijuavyo ni kuwa wale wenye kujuzusha mwanaume kumwangalia mwanamke ajinabi na mikono yake hawana dalili kutoka katika Qur-aan na Sunnah isipokuwa zifuatazo:

1- Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ

“… na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika [kwa kuwa hakuna njia ya kuyaficha]… “[1]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Bi maana uso, vitanga vya mikono na pete.”

Imepokea al-A´mash kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr kutoka kwake. Tafsiri ya Swahabah ni hoja kama tulivyotangulia kusema.

2- Abu Daawuud amepokea katika “as-Sunan” yake kutoka kwa ´Aiashah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na alikuwa amevaa mavazi ya kubana ambapo Mtume akageuka na kusema:

“Ee Asmaa´! Wakati mwanamke anapobaleghe hatakiwi kuonesha chochote isipokuwa hiki na hiki” na akaashiria uso na vitanga vyake vya mikono.”[2]

3- al-Bukhaariy na wengine wamepokea kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) jinsi kaka yake al-Fadhwl alivokuwa amekaa kwenye mnyama nyuma ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati wa Hajj ya kuaga. Pindi mwanamke kutoka Khath´am alipokuja akaanza kumtazama na yeye [mwanamke huyo] anamtazama. Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akageuza uso wake upande mwingine[3]. Katika hili kuna dalili kuwa mwanamke alionesha uso wake.

4- al-Bukhaariy na wengine wamepokea kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) juu ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaswalisha kwake watu swalah ya idi na akawapa mawaidha na kuwakumbusha kisha akaenda kwa wanawake akawapa mawaidha na kuwakumbusha. Akasema:

“Enyi wanawake! Toeni swadaqah! Hakika nyinyi ndio wengi Motoni.” Ndipo akasimama mmoja katika wanawake bora na alikuwa na mashavu ya kupauka… “[4]

Lau uso wake ungelikuwa hauko wazi basi mtu asingelijua ana mashavu ya kupauka.

Nijuavyo ni kwamba hizi ndio dalili kuwa inajuzu kwa mwanamke kuonesha uso wake wanaume ajinabi.

[1] 24:31

[2] Abu Daawuud (4104).

[3] al-Bukhaariy (1513) na Muslim (1334).

[4] Muslim (885).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hijaab, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 26/03/2017