Shaykh Bakr amesema:

“Kwa kichwa cha khabari chako “Sayyid Qutwub anaenda kinyume na wanachuoni na watu wa lugha juu ya maana ya “Laa ilaaha illa Allaah” na “Sayyid hatofautishi kati ya uola (Rubuubiyyah) na haki ya Allaah ya kuabudiwa (Uluuhiyyah)” umebomoa – bila ya kuthibitisha – yale yote aliyothibitisha Sayyid (Rahimahu Allaah) katika mafunzo ya Tawhiyd na yale yanayoipelekea yanayozungumzia maisha yake marefu. Yote uliyotaja yanayovunjwa na neno moja tu, nalo ni: Upwekeshwaji wa Allaah katika kuhukumu ni katika mambo yanayopelekewa na Tawhiyd. Sayyid (Rahimahu Allaah) alilitilia mkazo mkubwa hili pindi alipoona namna ambavyo ujasiri huu unavyofuta hukumu ya Allaah katika mahakama na jinsi badala yake kanuni za wanaadamu zilivyochukua nafasi. Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba Ummah wa Kiislamu haukuwa unajua ujasiri huu kabla ya mwaka 1342.”

Kutosheka na kutaja kichwa cha khabari peke yake bila ya kuingia ndani ya maandiko na kuyajadili kielimu ni kitu ambacho kimekuwa ni chenye kuzoeleka katika barua hii. Ni kana kwamba unayakimbia mbali. Baada ya hapo unarudi unanyata kwenye vichwa vya khabari ambavyo unashambulia kwavyo kwa njia ya kutopambanua na ya ujumla. Kwa sababu malengo ya msingi ni kutaka kupata hisia za wafuasi wake na kuwafanya wahisi kuwa wameshinda hata kama unusuraji huu utakuwa ni dhidi ya haki na watu wake. Lau kweli malengo yangelikuwa ni kutafuta uadilifu na kubainisha haki, basi kamwe msingeingia katika hili kabisa.