21. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wako kati na kati katika mambo yote ya dini

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Katika mlango wa imani na dini wako kati na kati baina ya Haruuriyyah na Mu´tazilah, kati ya Murji-ah na Jahmiyyah. Wako kati na kati katika mlango wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kati ya Raafidhwah na Khawaarij.

MAELEZO

Haruuriyyah na Mu´tazilah – Haruuriyyah ni Khawaarij. Wameitwa “Haruuriyyah” kwa sababu walikusanyika pahali ´Iraaq panapoitwa “Haruuraa´”. Walikusanyiko huko kwa sababu ya kuwapiga vita waislamu. Ndipo wakaitwa “Haruuriyyah”. Kila mwenye kuitakidi madhehebu yao anaitwa “Haruuriy” kwa sababu atakuwa juu ya madhehebu ya Haruuriyyah.

Mu´tazilah ni wafuasi wa Waaswil bin ´Atwaa´ ambaye alijitenga na kikao cha al-Hasan al-Baswriy.

Himdi zote njema anastahiki Allaah kuona kuwa Ahl-us-Sunnah wako kati na kati katika mambo yote ya dini. Wako kati kwa kati baina ya kuchupa mpaka na kuzembea, kuvuka mpaka na kuchukulia wepesi mambo. Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

كَذَٰلِكَ جَعَلْنَاكُمْ أُمَّةً وَسَطًا

“Ndivyo hivyo Tumekufanyeni ummah kati na kati na adilifu.”[1]

Ukatikati ni uadilifu na ubora. Inahusiana na ukatikati baina ya pande mbili; upande wa uchupaji mpaka na upande wa uchukuliaji wepesi. Khawaarij walichukua upande wa uchupaji mpaka. Murji-ah wakachukua upande wa uzembeaji. Himdi zote anastahiki Allaah kuona kwamba Ahl-us-Sunnah wako kati na kati baina ya hawa na wale.

[1] 02:143

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 40
  • Imechapishwa: 10/03/2021