Suala la pili: Machukizo ya swawm

Yapo baadhi ya mambo yaliyochukizwa kwa mfungaji ambayo yanaweza kuijeruhi funga yake na kupunguza ujira wake. Nayo ni yafuatayo:

1- Kupandisha sana maji puani na kupalizia. Hayo ni kwa kuchelea maji yasije kuingia tumboni mwake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Fanya kishindo katika kupalizia isipokuwa kama utakuwa umefunga.”[1]

2- Kubusu kwa ambaye yanaamka matamanio yake muda wa kuwa sio katika wale ambao wanaweza kuzimiliki nafsi zao. Katika hali hiyo imechukizwa kwa mfungaji kumbusu mke wake au kijakazi wake. Kwa sababu jambo hilo linaweza kuamsha matamanio yake ambayo yanaweza kupelekea kuiharibu funga yake kwa kutokwa na manii au jimaa.

Akijiamini nafsini mwake kutoharibika funga yake basi hakuna neno. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akibusu hali ya kuwa amefunga. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Alikuwa ni mwenye kumiliki zaidi haja zake kuwashinda.”[2]

Kadhalika anatakiwa kujiepusha na yale yote yanayochochea na kuamsha matamanio yake. Kama kwa mfano kuendeleza kumtazama mke, kijakazi au kufikiria jambo la jimaa, kwani jambo hilo linaweza kupelekea kutokwa na manii au kufanya jimaa kabisa.

3- Kumeza makohozi. Kwa sababu yanafika tumboni na anapata nguvu kwayo. Ukiongezea pia uchafu na madhara yanayoweza kupatikana kwa sababu ya kitendo hichi.

4- Kuonja chakula pasi na mtu kuhitaji kufanya hivo. Ikiwa amefanya hivo kwa sababu ya haja – kama mfano wa mpishi na anahitaji kuonja chumvi na mfano wake – hakuna neno. Lakini achukue tahadhari kusiwe chochote katika hayo kitachofika kooni mwake.

[1] at-Tirmidhiy (788) ambaye ameisahihisha, an-Nasaa´iy (01/66), Ibn Maajah (407). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-in-Nasaa´iy” (85).

[2] al-Bukhaariy (1927) na Muslim (1106).

  • Mhusika: Nukhbatin minal-´Ulamaa´
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fiqh-ul-Muyassar, uk. 160-161
  • Imechapishwa: 28/04/2020