20. Shari´ah imetahadharisha juu ya kuchupa mipaka na ikaamrisha kumtakasia nia Allaah pekee

Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wameonya juu ya suala zima la kuchupa mipaka. Amesema (Ta´ala):

قُلْ يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لَا تَغْلُوا فِي دِينِكُمْ

“Sema: “Enyi Ahl-ul-Kitaab! Msivuke mipaka katika dini yenu.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msinisifu sana kwa kupitiliza kama walivomsifu sana kwa kupitiliza manaswara ´Iysaa, mwana wa Maryam. Hakika mimi ni mja wa Allaah. Hivyo semeni “Mja na Mtume wake.”[2]

Allaah (Ta´ala) ametuamrisha kumuomba Yeye pekee pasi na mkatikati. Ni mamoja awe walii au mwengine. Ametuahidi kwamba atatuitikia – Yeye si mwenye kwenda kinyume na ahadi Yake. Amesema (Subhaanah):

وَقَالَ رَبُّكُمُ ادْعُونِي أَسْتَجِبْ لَكُمْ

”Mola wenu amesema: “Niombeni Nitakuitikieni.”[3]

وَإِذَا سَأَلَكَ عِبَادِي عَنِّي فَإِنِّي قَرِيبٌ ۖ أُجِيبُ دَعْوَةَ الدَّاعِ إِذَا دَعَانِ

“Watakapokuuliza waja Wangu kuhusu Mimi, basi Mimi ni niko karibu; naitikia du’aa ya muombaji anaponiomba.”[4]

ادْعُوا رَبَّكُمْ تَضَرُّعًا وَخُفْيَةً

“Muombeni Mola wenu kwa unyenyekevu na kwa siri.”[5]

فَادْعُوهُ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

”… basi muombeni hali ya kumtakasia Yeye dini.”[6]

Hali kadhalika Aayah zote utaona kuwa ndani yake kuna maamrisho ya kumuomba Yeye moja kwa moja pasi na ukatikati wa yeyote. Mawalii na waja wema ni waja wahitaji na ni mafakiri mbele ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ

“Hao wanaowaomba [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia [na] kumkurubia kadri wanavyoweza na wanataraji rehema Zake na wanakhofu adhabu Yake.”[7]

al-´Awfiy amepokea kutoka kwa Ibn ´Abbaas ambaye amesema kuhusiana na Aayah:

“Washirikina walikuwa wakisema: “Tunawaabudu Malaika, al-Masiyh na al-´Uzayr.” Ndipo Allaah (Ta´ala) akasema:

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ

“Hao wanaowaomba… “

bi maana Malaika ambao wanawaabudu wanafanya bidii kutafuta ukuruba kwa Allaah. Malaika hawa wanatarajia rehema za Allaah na wanakhofu adhabu Zake. Ambaye hali yake ndio hiyo hastahiki kuombwa pamoja na Allaah.”[8]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Aayah ni yenye kuenea. Inawahusu wale wote ambao walikuwa wanaabudiwa badala ya Allaah. Ni mamoja walikuwa ni Malaika, majini au watu. Aayah ni yenye kumzungumzisha kila yule mwenye kuombwa badala ya Allaah. Mwenye kuombwa huyo anatafuta njia ya kumfikisha kwa Allaah, anatarajia rehema Zake na anakhofu adhabu Zake. Hivyo kila mwenye kumuomba maiti au aliye mbali, Mtume au mja mwema, kwa tamko la kuomba uokozi au jengine, basi Aayah imemgusa kama ambavo inamgusa yule mwenye kuwaomba Malaika na majini.”[9]

[1] 05:77

[2] al-Bukhaariy (06/478) pamoja na ”al-Fath”.

[3] 40:60

[4] 02:186

[5] 07:55

[6] 40:65

[7] 17:57

[8] Tafsiyr-ul-Kariym al-´Adhwiym (03/46).

[9] Majmuu´-ul-Fataawaa (11/529) ya Shaykh-ul-Islaam.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan Haqiyqat-it-Tawhiyd, uk. 34-37
  • Imechapishwa: 29/03/2019