20. Njia ambazo imetajwa mikono na macho


Mikono na macho iliyoegemezwa kwa Allaah (Ta´ala) katika Qur-aan na Sunnah imetajwa kwa njia ya umoja, uwili na wingi. Mfano wa umoja, Allaah (Ta´ala) amesema:

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ

“Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni Muweza.”[1]

وَلِتُصْنَعَ عَلَىٰ عَيْنِي

“… na ili ulelewe Machoni Mwangu.”[2]

Kuhusiana na wingi, Allaah (Ta´ala) amesema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ

“Je, hawaoni kwamba Sisi Tumewaumbia kutokana na yale iliyofanya Mikono Yetu wanyama wa mifugo basi wao wanawamiliki.”[3]

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا

Inatembea kwa Macho Yetu.”[4]

Ama uwili, Allaah (Ta´ala) amesema:

بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ

“Bali Mikono Yake imekunjuliwa.”[5]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Pindi mja anaposimama kwa ajili ya kuswali, basi husimama kati ya macho mawili ya Mwingi wa Rahmah.”

Hivi ndivyo ilivyotajwa katika “Mukhtaswar-us-Swawaa´iy al-Mursalah” kutoka kwa ´Atwaa´, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bila ya kutaja ipo wapi[6]. Macho hayakutajwa katika Qur-aan kwa njia ya uwili. Njia hizi tatu ndivyo mikono na macho yalivyotajwa katika Qur-aan na Sunnah.

Njia hizi tatu zinaoanishwa ifuatavyo:

Njia ya umoja haipingani na uwili wala wingi. Kwa sababu umoja uliyoegemezwa ni wenye kuenea na unafunika mikono na macho yote yaliyothibiti kwa Allaah sawa ikiwa ni njia ya umoja au wingi.

Kuhusiana na kujumuisha kati ya uwili na wingi, hakuna mgongano kabisa endapo tutasema kuwa uwili ndio idadi ya chini kabisa ya wingi. Na endapo tutasema kuwa herufi tatu ndio idadi ya chini ya wingi, kama ambavyo inajulikana, basi tunajua kuwa lengo lililokusudiwa kwa wingi sio idadi ambayo ni zaidi ya mbili. Lengo lililolengwa ni utukuzwaji wenye kuendana na zile sifa zilizoegemezewa. Sifa hizi zimeegemezwa “Sisi” zikilenga utukuzwaji. Pindi Allaah alipotajwa kwa njia ya wingi, ni jambo lenye kuedana sifa Zake pia zilizoegemezwa Kwake kutajwa kwa njia ya wingi. Wingi unatimiza makusudio ya utukuzaji na uadhimisho zaidi kuliko njia ya umoja na uwili. Hivyo basi, ikiwa Allaah na zile zifa anazoegemezewa zitatajwa kwa njia ya wingi, ndipo hupatikana utukuzaji ulio bora zaidi.

[1] 67:01

[2] 20:39

[3] 36:71

[4] 54:14

[5] 05:64

[6] Tazama as-Swawaa´iq (1/256).