Istihaadhah ni kutirizika damu katika usiokuwa wakati wake kwa njia ya damu mbaya kutoka kwenye mshipa unaoitwa al-´Aadhil.

Mwanamke mwenye istihaadhah jambo lake ni lenye kutatiza kwa sababu damu ya istihaadhah hii hufanana na damu ya hedhi.

Ikiwa damu hiyo inashuka kwa kuendelea au kwa wakati mrefu, jambo gani analozingatia kuwa damu hiyo ni hedhi na ni jambo gani analozingatia kuwa damu hiyo ni istihaadhah ambayo kwayo hatoacha kufunga wala kuswali? Mwanamke mwenye damu ya istihaadhah anazingatiwa kwake hukumu za waliowasafi. Kujengea juu ya hayo yule mwenye istihaadhah ana hali tatu:

1 – Awe na ada inayotambulika kabla ya kupatwa na damu hii ya istihaadhah kwa njia ya kwamba kabla ya kupatwa na damu ya ugonjwa alikuwa akipata hedhi kwa siku tano au siku nane kwa mfano mwanzoni mwa mwezi au katikati yake. Hivyo mwanamke huyu anajua idadi yake na wakati wake. Mwanamke aina hii atakaa kwa kiwango cha ada yake na hivyo ataacha kuswali na kufunga na atazingatiwa kuwa na hukumu za hedhi. Ada yake ikimalizika basi ataoga na kuswali na damu yenye kuendelea ataizingatiwa kuwa ni damu ya ugonjwa. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Umm Habiybah:

“Jizuie kwa kiwango cha vile ilivyokuwa inakuzuia hedhi yako kisha uoge na uswali.”

Ameipokea Muslim.

Pia maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Faatwimah bint Hubaysh:

”Huo ni mshipa na wala si hedhi. Pale hedhi yako inapokuja basi acha swalah.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

2 – Asiwe na ada yenye kutambulika. Lakini hata hivyo damu yake ni yenye kupambanuka baadhi yake imebeba sifa za hedhi kwa njia ya kwamba ni nyeusi, nzito au ni yenye harufu mbaya na damu nyingine haikubeba sifa za hedhi kwa njia ya kwamba ni nyeusi, haina harufu mbaya wala si nzito. Katika hali kama hii ile damu ambayo imebeba sifa za hedhi itazingatiwa kuwa ni hedhi. Hivyo itambidi akae na aache kuswali na kufunga. Na ile damu nyingine itazingatiwa kuwa ni damu ya ugonjwa. Hivyo itambidi kuoga wakati itapoisha ile damu iliyobeba sifa za hedhi na kadhalika ataswali, atafunga na atazingatiwa kuwa ni msafi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Faatwimah bint Hubaysh:

“Ikiwa ni damu ya hedhi, ni nyeusi na inajulikana. Ikiwa ni hivyo basi jizuie kuswali. Na ikiwa ni nyingine tawadha na uswali.”

Ameipokea Abu Daawuud na an-Nasaa´iy. Ameisahihisha Ibn Hibbaan na al-Haakim.

Hapa kuna dalili inayoonyesha kwamba mwanamke mwenye istihaadhah anazingatia sifa ya ile damu ambayo atapambanua kwayo kati ya hedhi na damu nyingine.

3 – Akiwa hana ada inayotambulika wala sifa itayomuwezesha kati ya hedhi na damu nyingine. Katika hali hii atakaa muda mwingi wa hedhi ambao ni siku sita au siku saba kila mwezi. Kwa sababu hii ndio ada ya wanawake wengi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Himnah bint Jahsh:

“Hakika huo ni msukumo wa shaytwaan. Utakaa katika hedhi siku sita au saba kisha oga. Pale utakapoona umetwahirika kabisa, basi swali siku ishirini na nne au ishirini na tatu na ufunge na kuswali. Hakika hayo yatakutosheleza. Kadhalika fanya kama wanavyopata hedhi wanawake.”

Wameipokea watano na ameisahihisha at-Tirmidhiy.

Kwa kufupiza, kama tulivyotangulia kusema, ni kwamba mwanamke mwenye ada yake anarudishwa kwenye ada yake, mwenye kupambanua anarudishwa katika kutumia ule upambanuzi na yule mwenye kukosa hali mbili hizo atakaa hedhini siku sita au saba. Kufanya hivo ndani yake kuna kukusanya Sunnah tatu zilizopokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mwanamke mwenye damu ya ugonjwa. Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Alama zilizosemwa juu yake [mwanamke mwenye istihaadhah] ni sita: ima iwe ada; basi ada ni alama kubwa. Kwa sababu kimsingi ni kuweko hedhi na si kitu kingine. Au ni kupambanua kwa sababu damu nyeusi, nzito na yenye kutoa harufu ina haki zaidi ya kuwa hedhi kuliko ile damu nyekundu. Au kuzingatia ghalibu ya ada za wanawake. Kwa sababu kimsingi mmoja huingizwa ndani ya wenye kuenea ambao ndio mara nyingi. Alama hizi tatu zinafahamishwa na Sunnah na mazingatio.”

Halafu akataja alama zengine zilizosemwa.

Mwishoni akasema:

“Maoni sahihi ni kuzingatia alama zilizokuja kwenye Sunnah na kuzifuta nyenginezo.”

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 37-39
  • Imechapishwa: 29/10/2019