20. Mwenye busara na utani


1- Qataadah ameeleza kuwa Anas bin Maalik amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa na mtumwa akiitwa Anjashah ambaye alikuwa na sauti nzuri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Anjashah! Usizivunje glasi!”

Qataadah amesema:

“Akimaanisha wanawake wadhaifu.”

2- Ni wajibu kwa mwenye busara ajivutie kwa watu kwa kutania nao na aache kuonekana ni mwenye hasira.

3- Kuna aina mbili ya mzaha; mzaha wenye kusifiwa na wenye kusemwa vibaya. Utani wenye kusifiwa ni ule usiohusiana na yale yenye kumchukiza Allaah (´Azza wa Jall), madhambi wala kukata udugu. Utani wenye kusemwa vibaya ni ule unaosababisha uadui, unaondoa heshima, unakata urafiki, kumfanya mtu mbaya kumshambulia mtu na mtukufu kumchukia mtu.

4- Rabiy´ah amesema:

“Ninakutahadharisheni na mzaha. Hakika unaharibu mapenzi na unatia chuki kifuani.”

5- Ibn Hubayq amesema:

“Ilikuwa inasemwa mtu asifanye utani na mtukufu asije kukuchukia na wala asifanye utani na mbaya akaja kukushambulia.”

6- Ni ndugu wangapi wametengana kwa sababu ya mzaha? Ni wapenzi wangapi wamehamana kwa sababu ya mzaha? Yote yalianza kwa sababu ya mzaha.

7- al-Hakam amesema:

“Ilikuwa inasemwa mtu asigombane na rafiki yake na wala asifanye nae mzaha. Mujaahid alikuwa na rafiki aliyefanya naye utani. Hatimaye wote wawili wakapeana mgongo na hawakuzidishiana zaidi tu ya Salaam mpaka alipofariki.”

8- Kuna khatari mzaha ukasababisha mivutano. Ni wajibu kwa aliye na busara kujiepusha na hilo. Mizozo ni yenye kulaumiwa kwa hali zake zote. Pindi mtu anapojadili basi anafanye hivo ima na mtu ambaye ni mjuzi zaidi kuliko yeye – ni vipi atajadiliana na ambaye ni mjuzi zaidi kuliko yeye – au akajadiliana na ambaye ni mjinga zaidi kuliko yeye – ni vipi atajadiliana na ambaye anajua zaidi kuliko yeye?

9- Magomvi ni ndugu wa chuki kama ambavyo mijadala ndio dada wa uadui. Manufaa yake ni machache na shari yake ndio kubwa. Magomvi yanapelekea katika kutukanana na kutukanana kunapelekea katika kupigana na kupigana kunapelekea katika kumwaga damu. Kamwe mtu hajapatapo kujadili na mwengine isipokuwa magomvi yalizibadilisha nyoyo zao wote wawili.

10- Bilaal bin Sa´d amesema:

“Ukimuona mtu ni mwenye kutaka kulazimisha, mgomvi na mwenye kujiona kwa rai yake basi utambue kuwa imetimia hasara yake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Hibbaan al-Bustiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Rawdhat-ul-´Uqalaa’ wa Nuzhat-ul-Fudhwalaa’, uk. 77-79
  • Imechapishwa: 06/02/2018