20. Mwanamke kuonesha uso wake kunapelekea katika mchanganyiko

4- Wanawake kuchanganyika na wanaume. Pindi mwanamke anapoona kuwa ni kama mwanaume kwa kuonesha uso, hatoogopa kuchanganyika na kusongamana na wanaume. Hilo lina fitina kubwa ndani yake na ufisadi wenye kuenea. Siku moja wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotoka msikitini akaona wanaume wako pamoja na wanawake njiani. Hivyo akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwaambia wanawake:

“Tokeni. Hakika hamna haki ya kutembea kati kati ya njia. Tembeeni pembezoni mwa njia.”[1]

Ndipo wanawake wakaanza kutembea pembezoni kabisa na kuta mpaka mavazi yao yakagusana nazo. Haya yametajwa na Ibn Kathiyr wakati wa kufasiri Kauli ya Allaah (Ta´ala):

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ

“Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao… “[2]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema kuwa ni wajibu kwa wanawake kujifunika mbele ya wanaume ajinabi. Amesema:

“Allaah amegawanya mapambo sehemu mbili; mapambo yenye kuonekana na mapambo yasiyoonekana. Inajuzu kwa mwanamke kuonesha mapambo yake yenye kuonekana wanaume mbali na mume wake na ndugu wasiyoweza kumuuoa. Kabla ya Aayah yenye kuamrisha kujificha, Hijaab, wanawake walikuwa wakitoka bila ya mavazi ya juu. Wanaume walikuwa wanaweza kuona nyuso na mikono yao. Kipindi hicho ilikuwa bado inajuzu kuonesha uso na vitanga vya mikono na ilikuwa inajuzu kumtazama kwa vile ilikuwa inajuzu kwake kuonesha uso. Wakati Allaah alipoteremsha:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ

“Ee Nabii! Waambie wake zako na mabinti zako – na wanawake [wote] wa Waumini – ya kwamba [nje ya nyumbani] wajiteremshie mavazi yao ya juu.”[3]

wanawake wakajifunika kwa wanaume.”

Kisha akasema:

“Mavazi ya juu, Jilbaab, ni ile ambayo Ibn Mas´uud na wengine wanaita “mavazi ya kutia juu”. ´Awwaam wanaita kuwa ni “pazia”. Ni pazia kubwa inayofunika kichwa na mwili mzima. Ikiwa waliamrishwa kuvaa mavazi ya juu ili wasijulikane, hiyo ina maana uso unatakiwa kufunikwa au kuvishwa Niqaab, hivo ina maana ya kuwa uso na mikono ni katika mapambo ambayo hayatakiwi kuoneshwa mbele ya wanaume ajinabi. Mengineyo katika mavazi ya juu wanaume wanaweza kuona. Ibn Mas´uud ametaja suala la pili na Ibn ´Abbaas ametaja suala la kwanza.”

Kisha akasema:

“Kutokana na kauli sahihi ni kwamba hairuhusiwi kwa mwanamke kuonesha uso, mikono na miguu mbele ya wanaume ajinabi. Hata hivyo kabla ya kufuta ilikuwa inaruhusiwa kwake kuvionesha. Hivi sasa hakuna anachoruhusiwa kuonesha isipokuwa nguo tu.”[4]

Kwenye mjaladi huo huo amesema:

“Ama kuhusu uso, mikono na miguu, haruhusiwi tu kuvionesha wanaume ambao ni ajinabi. Hata hivyo anaruhusiwa kuwaonesha wanawake na ndugu wanaume wasioweza kumuoa.”[5]

Amesema pia:

“Msingi wa hili ni kwamba unajua kuwa Shari´ah iko na malengo mawili:

1- Kutofautisha kati ya wanaume na wanawake

2- Kumfunika mwanamke.”[6]

Haya ni maneno ya Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah. Kuhusiana na maneno ya Hanaabilah, nitataja maoni ya wanachuoni waliokuja nyuma. Mwandishi wa “al-Muntahaa” amesema:

“Ni haramu kwa mwanaume mhasi au mtowashi kumtazama mwanamke ajinabi.”

Kwenye kitabu “al-Iqnaa´” kuna:

“Ni haramu kumtazama mwanamke huru na ni haramu kutazama nywele zake.”

Mwandishi wa “ad-Daliyl” amesem:

“Kutazama kuna aina nane. Ya kwanza ni mwanaume ambaye kishabaleghe, hata kama ni mtowashi, kumtazama mwanamke ajinabi pasina haja. Haijuzu kwake kutazama chochote kwake, hata nywele zake za bandia.”

Shaafi´iyyah wanasema namna hii:

“Ikiwa ni mtazamo wa matamanio au kunakhofiwa fitina, basi ni haramu kabisa. Hakuna tofauti yoyote juu ya hilo. Na ikwia mtazamo sio wa matamanio na hakukhofiwi fitina yoyote, kuna kauli mbili juu ya suala hili. Zimetajwa na mwandishi wa kitabu “Sharh-ul-Iqnaa´” ambaye amesema:

“Kauli sahihi ni kuwa ni haramu kama ilivyotajwa katika “al-Minhaaj” na asli yake. Maimamu kwa makubaliano ya waislamu wote wamesema kuwa haipaswi kwa wanawake kutoka uso wazi na kwamba kutazama kunapelekea katika fitina na kuamsha matamanio.”

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ

“Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao… “[7]

Katika mazuri ya Shari´ah imekuja kuzuia kila ambacho kinapelekea katika madhara na mbali na hali zilizofafanuliwa.”

Katika kitabu “Nayl-ul-Awtwaar” mna:

“Waislamu wamekubaliana juu ya kwamba hairuhusiwi kwa wanawake kutoka nyuso wazi na khaswa pale ambapo madhambi ni mengi.”

[1] Abu Daawuud (5272).

[2] 24:31

[3] 33:59

[4] Majmuu´-ul-Fataawaa (22/110).

[5] Majmuu´-ul-Fataawaa (22/117-118).

[6] Majmuu´-ul-Fataawaa (22/152).

[7] 24:31

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hijaab, uk. 23-27
  • Imechapishwa: 26/03/2017