20. Mtoto anapaswa kufunzwa Uislamu

Watoto wanatakiwa kufunzwa dini ya Allaah. Haitakiwi kusubiri mpaka wawe wakubwa kwanza. Inatakiwa kutumia fursa ya wakati na umri wao ambapo watiliwe mkazo mambo ya dini, ´Aqiydah na uelewa. Wakishakuwa wakubwa wanakuwa wenye kushughulishwa na watapuuza jambo la kujifunza elimu. Mdogo sio kama mtu mkubwa. Mtoto mdogo ana wepesi zaidi wa kusoma. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwafunza wadogo kama ambavo anawafunza wakubwa. Alisema kumwambia ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) na kipindi hicho alikuwa mtoto mdogo:

“Ee Kijana! Nitakufundisha maneno: Muhifadhi Allaah Naye atakuhifadhi. Muhifadhi Allaah utamkuta mbele yako. Ukiomba, basi muombe Allaah, ukitafuta msaada, basi tafuta kutoka kwa Allaah. Jua ya kwamba ikiwa taifa zima litaungana kukunufaisha wewe kwa kitu, basi hutonufaika isipokuwa kwa kitu alichokwishakuandikia Allaah. Kadhalika wakikusanyika kukudhuru kwa chochote, basi howatokudhu isipokuwa tu kwa kitu alichokwishakuandikia. Kwani kalamu zimeshanyanyuliwa na sahifa zimeshakauka.”[1]

Pia alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Umar bin Abiy Salamah wakati walipokuwa wanakula pamoja:

“Ee kijana! Taja jina la Allaah, kula kwa mkono wako wa kulia na kula kile kilichoko mbele yako.”[2]

Anamfunza adabu za chakula; mtaje Allaah, kula kwa mkono wako wa kulia na  kula kile kilichoko mbele yako, usile kile kilicho mbele ya wengine. Namna hii watoto wanatakiwa kufunzwa. Wao wana wepesi zaidi ya kufunzika kuliko wakubwa.

[1] Ahmad (1/307) na at-Tirmidhiy (2516) ambaye amesema: ”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

[2] al-Bukhaariy (5376).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bayaan-ul-Ma´aaniy fiy Sharh Muqaddimati Ibn Abiy Zayd al-Qayrawaaniy, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 08/07/2021