20. Mke asimkasirikie mume wake

Miongoni mwa haki za mume juu ya mke wake ni yeye kufanya bidii kutomkasirikia wala kukasirikiwa. Akimkasirikia au akikasirikiwa ahakikishe anamridhisha. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanawake wenu ambao ni wanawake bora wa Peponi ni yule mwenye mahaba, mwenye rutuba na mwanamke mwenye kujirudi ambaye, pindi anapoudhika au anapoudhiwa, anaweka mkono wake kwenye mkono wa mume wake na kusema: “Ninaapa kwa Allaah kuwa sintosinzia mpaka utaporidhia.”[1]

Wakati anapoudhika kunamaanishwa pindi anapomuudhi mume wake. Wakati anapoudhiwa kunamaanishwa pindi anapoudhiwa na mume wake. Katika upokezi mwingine imekuja: “wakati anapokasirika”.

Mwanamke mwema alobarikiwa huchelea mume wake kumkasirikia. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu watatu Swalah zao hazivuki masikio yao; mja ambaye yuko katika ukimbizi mpaka arudi, mwanamke anatumia usiku wakati mume wake amemkasirikia na kiongozi anayewaongoza watu ilihali wanamchukia.”[2]

Wakati mwanamke alobarikiwa anapomkasirikia mume wake hamsusi. Hajiweki mbali na kitanda cha mume wake kwa hali yoyote. Haijalishi kitu hata kama atakuwa na khasira. Kwa sababu anajua kuwa Mtume mkweli na mwenye kusadikishwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakati mwanamke atatumia usiku katika hali ya kujiweka mbali na kitanda cha mume wake Malaika humlaani mpaka pale ataporudi.”[3]

Ukoje msimamo wa wanawake juu ya hili? Ukoje msimamo wa wanawake wa leo juu ya hili? Wakati wanawake wa leo wanapowakasirikia waume zao wanapaki mabegi yao na wanaenda kwa familia zao. Wanabaki huko kwa masiku. Familia zao zinawazuia waume zao na wanawanyima haki zao. Hawawahamasishi kurudi kwa waume. Hawawatii adabu wala kuwafunza. Je, wanawake hawa wa sasa hawakujitenga mbali na vitanda vya waume zao? Ninaapa kwa Allaah kuwa yeye ni mke na amejiweka mbali na kitanda cha mume wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemwambia:

“Wakati mwanamke atatumia usiku katika hali ya kujiweka mbali na kitanda cha mume wake Malaika humlaani mpaka pale ataporudi.”

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) vilevile:

“Mtu atapomwita mwanamke wake kwenye kitanda chake na akaacha kuja na akawa amemkasirikia usiku, Malaika humlaani mpaka asubuhi.”[4]

[1] an-Nasaaiy (5/9139) na at-Twabaraaniy (12/12468). Muundo ni wa an-Nasaaiy.

[2] at-Tirmidhiy (360) ambaye amesema: ”Nzuri na geni.” Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb” (487).

[3] al-Bukhaariy (5194) na Muslim (1436). Muundo ni wa al-Bukhaariy.

[4] al-Bukhaariy (3238) na Muslim (1436). Muundo ni wa al-Bukhaariy.

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliym ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Haqq-uz-Zawjayn, uk. 32-34
  • Imechapishwa: 24/03/2017