20. Masharti ya Mujtahid yasiyopatikana hata kwa Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa)

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Mujtahid ni yule mwenye kusifika na sifa kadhaa na kadhaa. Sifa ambazo huenda zisipatikane kwa ukamilifu hata kwa Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

MAELEZO

Wameweka masharti ya Mujtahid mutlaq ambayo hayapatikani kikamilifu kwa wale ambao ni wabora wa watu mfano wa Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Ni masharti ambayo wameyaweka wao wenyewe. Allaah (Ta´ala) amesema:

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ

“Je hawaizingatii Qur-aan?” (04:82)

Hili linawahusu waislamu wote. Kila mmoja anajua katika Qur-aan kile ambacho Allaah amemfanyia wepesi. Ambaye si msomi anaelewa kile anachokiweza, mwanafunzi anaelewa kile anachokiweza na mwanachuoni aliyebobea anaelewa kile anachokiweza:

أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌ بِقَدَرِهَا

“Ameteremsha kutoka mbinguni maji [mvua] na mabonde yakatiririka [maji] kwa kadiri yake.” (13:17)

Kila bonde kunatiririka maji kwa kadiri yake. Hali kadhalika elimu ambayo Allaah ameiteremsha. Kila moyo unachukua kutoka katika elimu hiyo kwa kadiri yake. Kuna moyo wa ambaye si msomi, moyo wa mwanafunzi, moyo wa mwanachuoni na moyo wa mwanachuoni aliyebobea zaidi katika elimu. Kila mmoja anachota kwa kiasi na fahamu alizompa Allaah. Kusema kuwa hakuna mwenye kuifahamu Qur-aan isipokuwa yule ambaye ni Mujtahid mutlaq, maneno haya sio sahihi.

Wanasema kuwa kule kujaribu kuifahamu Qur-aan ni katika kujikalifisha kwa kitu kisichowezekana. Masharti yaliyotajwa na wanazuoni na kusema kuwa ni lazima kwa Muftiy ayatimize, wanakusudia Mujtahid mutlaq na si kwamba wanakusudia kuwa ni lazima ayatimize kila yule ambaye anataka kuizingatia Qur-aan na kustafidi kutoka ndani yake. Isitoshe jengine ni kwamba hayo ni masharti ya kunyofoa hukumu zisizokuwa wazi na sio masharti ya kufahamu mambo yaliyo wazi kama mfano wa Tawhiyd, shirki, mambo ya wajibu yaliyo wazi na mambo ya haramu yaliyo wazi.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 41
  • Imechapishwa: 19/05/2021