20. I´tiqaad za Ahl-ul-Bid´ah juu ya Qur-aan

Jahmiyyah wanakanushaji na wapindukaji wamekanusha majina na sifa zote za Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ikiwa ni pamoja na maneno ya Allaah, kukiingia Qur-aan tukufu.

Mu´tazilah wamesema wazi kwamba Qur-aan imeumbwa. Kwa mtazamo wao wanaona kuwa Qur-aan imeumbwa na Allaah kama jinsi alivoumba viumbe vyengine vyote. Wanawatatiza watu kwa Aayah za Qur-aan ilihali ukweli wa mambo si dalili. Wanawababaisha wale wajinga na matokeo yake wakawafuata au angalau kwa uchache wakawafanya kudangana. Miongoni mwa hoja wanazotumia ni maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ

”Allaah ni muumbaji wa kila kitu.”[1]

Wamesema kwamba Aayah imetajwa kwa ujumla na kwa mtazamo wao eti muqtadha isiyojulikana inapelekea ujumla, kukiwemo Qur-aan. Hivyo Qur-aan ni katika vile vyote vilivyoumbwa. Matokeo yake upambanuzi na ubabaishaji huu ukawakinaisha wale wote ambao ni wajinga ambapo wakawatii maovu haya makubwa.

Kuhusu Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah, ni wenye kuelewa maana ya Qur-aan vyema kuliko watu wa Bid´ah. Wakawaraddi Mu´tazilah na misingi yao na vifaranga vyao waziwazi. Kwa ajili hiyo ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kwamba mtu ajadiliane na Ahl-ul-Ahwaa´ kwa Sunnah. Kwa sababu Ahl-us-Sunnah ni wajuzi zaidi wa Kitabu cha Allaah kuliko Ahl-ul-Bid´ah na upotevu. Ni kweli kwamba “kila” ni yenye kuenea, lakini kuenea kwake kunategemea na kile chenye kuegemezwa kwalo. Miongoni mwa hoja zao ni maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

تُدَمِّرُ كُلَّ شَيْءٍ بِأَمْرِ رَبِّهَا فَأَصْبَحُوا لَا يُرَىٰ إِلَّا مَسَاكِنُهُمْ

“Unaangamiza kila kitu kwa amri ya Mola wake. Wakapambaukiwa hayaonekani isipokuwa majengo yao.”[2]

Hapa kulibomolewa kila kitu na majengo yakavuliwa katika ueneaji huo. Kadhalika Allaah ameumba kila kitu kinachostahiki kuumbwa, lakini dhati ya Allaah, majina na sifa Zake havikuumbwa. Kwa ajili hiyo mambo yakabainika kwa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah iliyoanza Kwake na Kwake ndiko ikarudi.

Wakaikataa na kuipinga ´Aqiydah ya Jahmiyyah na Mu´tazilah. Ashaa´irah na wenzao Kullaabiyyah na Maaturiydiyyah wanasema kuwa maneno ya Allaah ni manaa na yamesimama kwenye nafsi na kwamba hayana herufi, sauti wala matamshi. Wamejengea juu ya vipimo visivyotakiwa kutumiwa juu ya majina na sifa za Allaah. Ni kipi kimechowafanya kusema hivo? Ni kwa sababu wanaona kwamba maneno ni lazima yatoke kwenye ulimi, midomo na koo vitu ambavyo ni mwili. Kwa mtazamo wao wanaona kwamba wakithibitisha maneno basi inapelekea kwamba Allaah anasifika kwa viungo hivi vya mwili, jambo ambalo linapelekea kwamba Allaah na kiwiliwili, jambo ambalo linapelekea kwamba wanatumbukia katika ukafiri. Kwa hivyo wakalazimika kufasiri hivo ili wasije kutumbukia kwenye ukafiri, kwa sababu Allaah ametakasika kutokamana na miili. Kwa msemo mwingine Allaah hana mwili na viungo hivi vya mwili. Dalili yao wanayotegemea ni akili zao dhaifu. Kuhusu Qur-aan na Sunnah viko dhidi yao. Kwa mfano Allaah amesema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.”[3]

Hakuna chochote kinachofanana na Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) inapokuja katika dhati, majina, sifa na matendo Yake – Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona. Haifai kumlinganisha na viumbe Wake kwa hali yoyote ile. Haitakiwi kusema kwamba maneno Yake yanapelekea katika hiki na kile. Maneno Yake hayatakiwi kukanushwa. Yeye ndiye Mwenye ukamilifu usiyokuwa na kikomo. Yeye ni Mkubwa, Aliye juu. ´Abdullaah bin ´Abbaas (Radhiya Allaah ´anhumaa) amesema:

“Mbingu na ardhi saba kwenye kiganja cha Mwingi wa huruma si chochote isipokuwa ni kama mbegu ya hardali kwenye mkono wa mmoka wenu.”

[1] 39:62

[2] 46:25

[3] 42:11

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 72-74
  • Imechapishwa: 09/10/2019