20. Inajuzu kwa mume kufanya al-´Azl

18- Kujuzu kwa al-´Azl

Inajuzu kwake kuchopoa [dhakari yake] kabla ya kushusha maji yake. Kuna Hadiyth juu ya hilo:

1- Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Tulikuwa tukifanya al-´Azl[1] na huku Qur-aan ikiteremka.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Tulikuwa tukifanya al-´Azl wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hilo likamfikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wala hakutukataza.”[2]

2- Kuna mtu alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mimi nina mjakazi na mimi humfanyia al-´Azl. Mimi nataka kile anachotaka mwanamume. Mayahudi wamedai kuwa al-´Azl ni aina ndogo ya kuua.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Wamesema uongo mayahudi. Wamesema uongo mayahudi. Iwapo Allaah angelitaka kumuumba basi usingeliweza kumzuia.”[3]

3- Jaabir amesimulia ya kwamba kuna mwanamume alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mimi nina mjakazi ambaye ni mtumishi wetu anayetumwagilia maji kwenye miti ya mitende. Nimemjamii na sipendi anizalie mtoto. Akamwambia: “Mfanyie al-´Azl ukitaka. Lakini kitakuja kile ambacho amekadiriwa. Mtu yule akapotea kisha baada ya muda akarudi na kusema: “Yule mjakazi ameshika mimba.” Akamwambia: “Nilikwambia kuwa atajiwa na kile alichokadiriwa.”[4]

[1] Imekuja katika “al-Fath”:

“al-´Azl ni kule kuchopoa baada ya kuingiza kwa ajili ya kumwaga nje ya tupu ya mwanamke.”

[2] Ameipokea al-Bukhaariy (09/250) na Muslim (04/160). Upokezi wa pili ni wake. Ameipokea pia an-Nasaa´iy katika “al-´Asharah” (01/82), at-Tirmidhiy (02/193) ambaye ameisahihisha. Ameipokea pia al-Baghawiy katika “Hadiyth ´Aliy bin al-Ja´d (02/76/08).

[3] Ameipokea an-Nasaa´iy katika “al-´Asharah” (01/81-2), Abu Daawuud (01/238), at-Twahaawiy katika “al-Mushakkil” (02/371), at-Tirmidhiy (02/193), Ahmad (03/33), (51) na (53) kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh.

[4] Ameipokea Muslim (04/160), Abu Daawuud (01/339), al-Bayhaqiy (07/229), Ahmad (03/312) na (386).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Aadaab-uz-Zafaaf, uk. 130-133
  • Imechapishwa: 12/03/2018