Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Hakuna tofauti katika mambo yote haya yanayochengua Uislamu kati ya mwenye kufanya mzaha, mwenye kukusudia na mwenye kuogopa. Isipokuwa tu yule aliyetenzwa nguvu. Yote haya ni katika [mambo] makubwa ambayo yanakuwa ni yenye khatari na mara nyingi hutokea. Hivyo basi, inatakikana kwa muislamu kutahadhari nayo na ayaogope juu ya nafsi yake. Tunajikinga kwa Allaah kwa yanayopelekea katika ghadhabu Zake na adhabu Yake kali.

Swalah na amani zimwendee kiumbe Chake bora Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

MAELEZO

Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) anasema kuwa hakuna tofauti katika mambo haya yanayochengua Uislamu kati ya anayefanya mzaha, mwenye kukusudia kweli na mwenye kuogopa. Isipokuwa tu mtenzwa nguvu. Vichenguzi hivi ndiyo vya khatari sana na vinavyotokea kwa wingi kwa watu. Inampasa mtu ajihadhari navyo kwa sababu watu wengi hutumbukia ndani yake. Jengine ni kwa sababu khatari yake ni kubwa. Tunajilinda kwa Allaah kwa yanayopelekea katika hasira Zake na adhabu Yake kali.

Mtunzi (Rahimahu Allaah) amesema kuwa hakuna tofauti kati ya anayefanya mzaha, mwenye kukusudia kweli na mwenye kuogopa. Isipokuwa tu mtenzwa nguvu. Kwa hivyo hapa kuna hali mbalimbali:

1 – Mtu amefanya moja katika vichenguzi vya Uislamu hali ya kuwa anafanya mzaha. Kama mtu anayeichezea shere swalah au dini kwa njia ya mzaha na kejeli. Huyu anakufuru.

2 – Mwingine amefanya moja katika vichenguzi vya Uislamu hali ya kuwa ni mwenye kumaanisha kweli. Kama mfano wa anayeifanyia dhihaka dini hali ya kuwa ni mwenye kumaanisha kweli. Huyu anakufuru.

3 – Mwenye kufanya moja katika vichenguzi vya Uislamu kwa kuchelea juu ya nafsi yake, mali yake au mtoto wake. Huyu anakufuru hata kama atakuwa ni mwenye kuogopa. Kama mfano wa mwenye kuutukana Uislamu mbele ya mtu ili mali yake iweze kubaki na isichukuliwe. Kwa sababu anachelea ikiwa hatotukana Uislamu basi mali yake itachukuliwa. Lau atachelea mali yake, nafsi yake au mtoto wake anakufuru.

4 – Mwenye kukirihishwa hali ya kuwa moyo wake umetua kwenye ukafiri anakufuru. Kwa mfano mtu ambaye amewekewa upanga shingoni mwake na kuambiwa ima ukufuru vinginevyo tunakuua. Mtu ambaye yuko katika hali kama hii akitamka neno la kufuru na wakati huohuo moyo wake umetua juu ya imani hakufuru. Lakini ikiwa amelazimishwa na wakati huohuo moyo wake umetua juu ya ukafiri, basi anakufuru. Kwa mfano mtu amewekewa upanga shingoni na kuambiwa akufuru na vinginevyo wanamuua, akitamka neno la kufuru na huku moyo wake umetua juu ya imani, hakufuru.

Kwa hivyo mwenye kufanya moja katika mambo haya yanayochengua Uislamu hali ya kuwa ni mwenye kufanya mzaha, anamaanisha kweli au ni mwenye kuogopa anakufuru. Isipokuwa yule mwenye kutenzwa nguvu. Akikufuru pamoja na kuwa anachukia hilo na kwa sharti moyo wake uwe umetua juu ya imani [hakufuru]. Kwa kufupisha ni kwamba hapa tuna hali tano:

1 – Yule mwenye kufanya kufuru au moja katika yanayochengua Uislamu ilihali ni mwenye kufanya mzaha anakufuru.

2 – Anayefanya kufuru au moja katika yanayochengua Uislamu hali ya kuwa ni mwenye kumaanisha kweli anakufuru.

3 – Mwenye kufanya kufuru kwa kuogopa – na jambo la kutokukufuru liko ndani ya uwezo wake – anakufuru.

4 – Mwenye kufanya kufuru kwa kutenzwa nguvu na wakati huohuo moyo wake umetua juu ya ukafiri – kwa maana ya kwamba alipokirihishwa ndipo akaazimia ukafiri – basi anakufuru.

5 – Mwenye kufanya kufuru kwa kutenzwa nguvu na wakati huohuo moyo wake umetua juu ya imani hakufuru.

Kwa hiyo hizi ni hali tano. Hali nne ambapo mtu anakufuru na moja hakufuru. Dalili yenye kuonyesha kwamba endapo anachelea juu ya nafsi yake, familia yake au mali yake ambapo kukamfanya kutamka maneno ya kufuru ili mali yake iweze kusalimika ya kwamba kitendo hicho pia ni ukafiri ni maneno Yake (Ta´ala):

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake [atapata adhabu] isipokuwa yule aliyetenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu ya imani.”

Hapa tunapata kuona kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amebagua hali moja peke yake; naye ni yule mwenye kutenzwa nguvu kwa sharti kwa sharti ya kwamba moyo wake uwe umetua katika imani:

إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ

“… isipokuwa yule aliyetenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu ya imani.”

Baada ya hapo Allaah (Subhaanah) akasema:

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake [atapata adhabu] isipokuwa yule aliyetenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu ya iymaan. Lakini aliyekifungulia ukafiri kifua chake, basi hao juu yao ni ghadhabu kutoka kwa Allaah na watapata adhabu kuu. Hivyo kwa sababu wao wamependelea uhai wa dunia kuliko wa Aakhirah.”[1]

Mwenye kukufuru kwa sababu ya mali yake, familia yake au mali yake amependelea na kuipa kipaumbele dunia juu ya Aakhirah, ameitanguliza dunia mbele kabla ya Aakhirah, ameitanguliza dunia mbele juu ya dini yake:

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Hivyo kwa sababu wao wamependelea uhai wa dunia kuliko wa Aakhirah.”

Akifanya ukafiri kwa kuchelea familia yake, mali yake au juu ya nafsi yake anakufuru. Hapewi udhuru kwa kuogopa kwake. Allaah (Ta´ala) amesema:

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ

“Hivyo kwa sababu wao wamependelea uhai wa dunia kuliko wa Aakhirah.”

Vivyo hivyo akifanya ukafiri kwa kufanya mzaha, kwa kukusudia kweli au kwa kutenzwa nguvu lakini moyo wake ukawa umetua juu ya ukafiri. Hakuna anayebaguliwa isipokuwa yule aliyelazimishwa na wakati huohuo moyo wake umetua katika imani.

Makusudio ya “kutenzwa nguvu” haina maana ya vitisho. Maana yake ni mtu akakirihishwa na kulazimishwa kikweli kwa njia ya kwamba akatiwa upanga juu ya shingo yake, akatishwa na mtu ambaye ni muuaji na anajua kuwa kweli huyu ni mwenye kutimiza ahadi yake papohapo endapo hatokufuru. Huyu ndiye mtenzwa nguvu tunayekusudia. Ikiwa atatamka au kufanya kitendo cha ukafiri na huku moyo wake umetua katika imani haitomdhuru kitu. Ama mtu kuogopa peke yake juu ya nafsi yake, familia yake au mali yake halimjuzishii kukufuru.

Tunamuomba Allaah (´Azza wa Jall) usalama na atufishe juu ya Uislamu. Tunajilinda kwa Allaah kutokana na kufuru, shirki, unafiki, khasara na tabia mabovu. Tunamuomba Allaah atuthibitishe katika dini Yake, atukinge na mitihani yenye kupotosha, atufishe katika Uislamu hali ya kuwa si wenye kugeuza wala kubadilisha. Hakika Yeye ndiye msimamizi na muweza wa hayo.

Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake Mtume wetu Muhammad, kizazi chake, Maswahabah zake na Taabi´uun.

[1] 16:106-107

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 57-60
  • Imechapishwa: 15/04/2023